Habari Mseto

Aliyeiba kanisani afariki kizuizini

September 1st, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

Mshukiwa aliyekamatwa akiiba katika kanisa moja katika kijiji cha Machagua kaunti ya Embu, alikufa akizuiliwa katika seli za polisi.

Henry Muchangi Ireri, 24 alikamatwa Alhamisi usiku na muumini katika kanisa la Jeshi la Wokovu na wakazi wakampeleka kituo cha polisi cha Kigumo ambapo alizuiliwa ili ahojiwe.

Hata hivyo, baada ya saa chache, Bw Ireri alianguka akiwa ndani ya seli na kufariki katika hali ambayo haikueleweka.

Mzee wa kanisa, Dominic Mugendi, alisema muumini alikuwa akichunga kanisa kufuatia visa vya wizi wa mali alipomuona mshukiwa akivunja chumba kinachotumiwa kama jiko kisha akaingia ndani.

Muumini huyo alimkabili mshukiwa na kupiga kamsa zilizovutia wakazi.

Bw Ireri alikimbia alipohisi kuwa maisha yake yalikuwa hatarini lakini alikamatwa na umati uliompeleka kituo cha polisi alipofia akizuiliwa.

Bw Mugendi alisema umati haukumpiga mshukiwa na kifo chake kinazua maswali mengi.

Naibu Mkuu wa polisi eneo la Embu mashariki Bw Michael Wachira alithibitisha kisa hicho na kusema mwili wa mwanamume huyo ulipelekwa mochari ya hospitali ya Runyenjes.

Ni kweli tuliondoa mwili wa mshukiwa kutoka seli na tukaupelea mochari,” alisema Bw Wachira na kuongeza kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichosababisha kifo cha Bw Ireri.

Aliwaambia wakazi waache kushuku na kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi. Kamanda wa polisi kaunti ya Embu Daniel Rukanga alisema alifahamishwa kisa hicho na atatoa taarifa baadaye.