Habari za Kitaifa

Aliyeiba mahindi ya Sh70 kuzima njaa afungwa jela miezi mitatu


MWANAUME mmoja alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na mahakama moja mjini Kakamega kwa kuiba mahindi ya thamani ya Sh70.

Bw Meshack Opandiandiati alitenda kosa hilo katika shamba moja katika kijiji cha Ematere katika Kaunti Ndogo ya Kakamega ya Kati.

Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Angeline Odawa ambapo alikiri mashtaka hayo.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo jioni ya Agosti 12, 2024, Bw Opandiandiati alinaswa akiiba mahindi kutoka kwa shamba la Bi Petronila Mwandihi katika kijiji cha Ematere.
Mahindi hayo yalikadiriwa kuwa na thamani ya Sh70.

Katika uamuzi wake, Bi Odawa alisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, akibainisha kuwa wizi, bila kujali kiwango kinachohusika, hauwezi kusamehewa.
“Wizi ni wizi, bila kujali umeibiwa kiasi gani. Sheria lazima iheshimiwe,” alieleza Hakimu.

Bw Opandiandiati alitozwa faini ya Sh10,000 la sivyo afungwe jela miezi mitatu.
Mshtakiwa, ambaye alionekana kuwa na shida, aliomba ahurumiwe akisema kwamba alikuwa aliiba mahindi kutokana na njaa.

“Sikuwa na nia ya kuiba, Mheshimiwa. Nilikuwa na njaa na sikuwa na chakula. Hivyo ndivyo nilivyoishia kuchuma mahindi ya kuchoma,” aliomba mahakama.

Hata hivyo, hakimu alisisitiza kwamba ingawa anaelewa changamoto za umaskini, hazifai kuwa kisingizio cha uhalifu.
“Lazima tutafute njia bora za kukabiliana na matatizo yetu, lakini kuvunja sheria hakuwezi kuwa suluhu,” alisema.