Habari Mseto

Aliyeingiza mabinti Wapakistani nchini kiharamu akamatwa

January 3rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWENYE KILABU kimoja jijini Nairobi alifikishwa mahakamani kwa kuwaingiza nchini kinyume cha wasichana wanane aliokuwa anawatumia kuwatumbuiza wateja wakibugia mvinyo.

Bw Safendra Kumar Sonwani , mwenye kilabu cha Balle Balle pamoja na meneja wake  Bw Mika Osicharo walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot.

Kiongozi wa mashtaka Bi Annette Wangia aliomba mahakama iwazuilie wawili hao hadi Ijumaa maafisa wa polisi wakamilishe uchunguzi ikiwa wasichana hao wanane wako na vibali  vya kuwaruhusu kuingia nchini.

Wasichana waliofumaniwa kilabuni. Picha/ Richard Munguti

“Naomba mahakama iwazuilie Mabw Sonwani na Osicharo kwa muda wa siku tano Polisi wabaini ikiwa wasichana waliokamatwa Januari 1, 2019 katika kilabu cha Balle Balle walikuwa na hati rasmi za kuwaruhusu kuingia nchini,” alisema Bi Wangia.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili Evans Ondieki aliyesema kuwa wasichana hao walipewa pasi spesheli na Waziri wa Utamaduni na Michezo Bw  Rashid Echesa.

“ Wasichana hawa walikubaliwa kuingia nchini na Bw Echesa. Nashangaa sababu Polisi wamewakamata Mabw Sonwani na Osicho kwa madai ya kuwalangua wasichana hao,” alisema Bw Ondieki huku akimkabidhi hakimu nakala za pasi maalum walizopewa wasichana hao.

Alisema muda wa pasi hizo utayoyoma Januari 18, 2019.

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot. Picha/ Richard Munguti

“Ikiwa idara moja ya Serikali haijuhi ile ingine vile imefanya basi inamaanisha Serikali haitekelezi kazi moja,” alisema  Bw Ondieki.

Mahakama iliombwa iwazuilie wasichana hao katika chumba maalum kwa vile ni mashahidi wa kulindwa.

“Ikiwa pasi hizi maalum zitabainika ni feki basi waishana hawa na Mabw Sonwani na Osichori watashtakiwa kwa makosa ya ulanguzi wa binadamu,” alisema Bw Wangia.

Mahakama iliamuru Mabw Sonwani na Osichori wazuiliwe hadi  kesho ripoti itakapotolewa kuhusu pasi za wasichana hao.