Aliyejeruhiwa akivuka feri Likoni kulipwa Sh418,000

Aliyejeruhiwa akivuka feri Likoni kulipwa Sh418,000

Na BRIAN OCHARO

MAHAKAMA Kuu ya Mombasa imeagiza kuwa mwanamume alipwe fidia ya Sh418,000 baada ya kujeruhiwa alipokuwa akivuka feri Likoni.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Njoki Mwangi, alikosoa korti ya chini iliyokataa kuamua kesi hiyo ya Bw John Gilbert Ouma, ambaye alivunjika mguu akiwa ndani ya kivuko hicho miaka mitano iliyopita.

Bw Ouma alishtaki Shirika la Huduma za Feri nchini (KFS) mnamo 2017 akitaka kulipwa fidia kwa kupata majeraha wakati akiwa ndani ya MV Kilindini.

Aliiambia korti kuwa ajali hiyo ilitokea Oktoba 17, 2016.Kulingana naye, wakati wakivuka kutoka Likoni kwenda kisiwani Mombasa, watu walianza kusukumana na kumsababisha aanguke kwenye sakafu ya chombo hicho.

“Nilikanyagwa na watu na kupata majeraha mabaya kwenye goti la mguu wangu wa kushoto,” aliiambia mahakama kupitia kwa wakili wake, Bw Simiyu Oduor.

Bw Ouma alisema kuwa kutokana na ajali hiyo ambayo alidai ilitokana na uzembe wa KFS, alivunjika mguu.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwangi alisema mahakama za mahakimu zina mamlaka ya kusikiliza na kuamua mizozo aina hiyo ikiletwa mbele yao

.Alifikia uamuzi huu baada ya kugundua kuwa korti ya hakimu ilifutilia mbali kesi iliyowasilishwa na Bw Ouma kwa hoja kwamba haikuwa na mamlaka ya kushughulikia suala hilo.

Hakimu mwanzoni alikuwa ameamuru Bw Ouma alipwe fedha hizo lakini baada ya KFS kupinga fidia hiyo, alifutilia mbali uamuzi huo kwa madai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuskiza mzozo huo.

KFS ilidai kuwa mizozo kuhusu feri inapaswa kutatuliwa na Mahakama Kuu wala sio mahakama za hakimu.

Shirika hilo lilidai kuwa ferri ni sawa na meli hivyo basi mahakama ya mahakimu haina mamlaka ya kutatua mizozo kuhusiana na vyombo hivyo.

Lakini Jaji Mwangi alitupilia mbali madai haya akibainisha kuwa kuna tofauti kati ya feri na meli.

  • Tags

You can share this post!

Waombaji wasiotenda

Nahitaji miaka 3 kuifahamu vyema idara – Jaji Mkuu...