Habari Mseto

Aliyejifanya polisi atiwa nguvuni

July 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wa kupambana na jinai, Ijumaa walimtia nguvuni mwanamume ambaye amekuwa akiambia wananchi kwamba yeye ni afisa wa polisi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) Ijumaa, Hirji Ramji Patel almaarufu Harish Daria alikamatwa akiwa na silaha mbalimbali pamoja na misokoto ya bangi.

“Maafisa wa upelelezi katika kituo cha polisi cha Gigiri walimtia nguvuni Hirji Ramji akiwa na silaha mbali mbali,” taarifa ya DCI ilisema.

Baada ya kumtia nguvuni mshukiwa, polisi walipata akiwa na bastola muundo wa Ceska, raudi 27 za risasi, makasha mawili ya risasi, Jaketi za kuzuia risasi, magwanda ya kijeshi, pingu na misokoto 25 ya bhangi na nguo za idara ya polisi.

Patel anayezuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu kujibu mashtaka mbalimbali.

Miongoni mwa mashtaka ni pamoja na kupatikana na bidhaa za Serikali, kudai – kuitisha – pesa kwa njia ya vitisho na kupatikana na mihadarati, afisi ya DCI ilisema.