Habari Mseto

Aliyejifanya wazimu akamatwa na misokoto ya bangi

April 24th, 2018 1 min read

Na WAIKWA MAINA

POLISI katika Kaunti ya Nyandarua, wanamzuilia mwanamume ambaye amekuwa akijifanya mwendawazimu mjini Ol Kalou, lakini anayeshukiwa kuwa muuzaji hatari wa dawa za kulevya mjini humo.

Jumatatu asubuhi, mwanamume huyo alipatikana na Sh33,900 kwenye msako wa wauzaji wa dawa za kulevya uliofanywa na maafisa wa polisi.

Polisi walisema mshukiwa, ambaye kila mtu mjini humfahamu kama mwenda wazimu, amekuwa akisafirisha dawa za kulevya.

Akiwa kituo cha polisi cha Ol Kalou, mwanamume huyo alionekana mwenye akili timamu na hata kuhesabu pesa zake zote na kuthibitisha zilikuwa sawa.

Alipatikana na pesa hizo kwenye msako ulioongozwa na mkuu wa polisi wa eneo hilo (OCPD), Wilson Kosgei, kwenye ukumbi mmoja wa kuchezea kamari ambao unashukiwa kuwa kituo cha kuuza dawa za kulevya.

“Nilipata habari kutoka kwa umma kwamba baadhi ya wauzaji wa dawa za kulevya huendesha shughuli zao kutoka hapo. Tulipowasili, niliagiza maafisa wangu kuwapekua vijana wote waliokuwa wakicheza pool. Tulishangaa kupata pesa nyingi kutoka kwa mwanamume ambaye amekuwa akijifanya wazimu,” alisema OCPD huyo.

Mwanahabari Ndichu Wainaina, aliyefika kituo cha polisi alisimulia jinsi alivyomsaidia mshukiwa dakika chache kabla ya kukamatwa kwa kumnunulia kikombe cha chai na andazi.

“Alinipata katika hoteli nilipokuwa nikinywa chai na marafiki na akaniomba nimnunulie kikombe cha chai. Kwa hivyo wakati huo alikuwa na pesa nyingi kuniliko. Nimeshangaa, nimekuwa nikimfahamu kama mtu asiye na akili timamu,” alisema Bw Ndichu.

Bw Kosgei alisema uchunguzi wa mwanzo umefichua kwamba mwanamume huyo amekuwa akitumiwa na mlanguzi mmoja wa mihadarati anayefahamika mjini humo kwa kusambaza dawa za kulevya.

Alisema mlanguzi huyo ameenda mafichoni.

“Pesa zilikuwa zimepangwa vizuri. Ananuka na tunaamini uvundo huo ndio silaha yake. Akiwa seli, yuko sawa kabisa na akili zake na hata amethibitisha pesa hizo zilirekodiwa katika kitabu cha matukio kituoni,” alieleza Bw Kosgei.