Habari Mseto

Aliyejiua kuhusu kansa alihofia upasuaji – Familia

August 12th, 2019 1 min read

Na JAMES MURIMI

MGONJWA wa kansa aliyejitoa uhai katika Kaunti ya Laikipia wiki iliyopita, alikuwa na wasiwasi mwingi na hofu ya kufanyiwa upasuaji tumboni Alhamisi hii katika Hospitali ya Nairobi South, familia yake imesema.

Huku wakiandaa mazishi ya Joseph Kibiriti Karuri, 66, katika boma lao lililo kijijini Mwaura, Kaunti Ndogo ya Laikipia Mashariki, jamaa zake walisema alidhoofika sana kiafya tangu alipoanza kuugua mwaka wa 2016.

Bi Millicent Wamuyu alisema babake alipatikana anaugua saratani mwaka wa 2018 katika Hospitali ya Consolata Mathari iliyo Nyeri wakati ugonjwa huo ulikuwa katika kiwango cha pili.

Hapo ndipo alianza kutatizika kimawazo na afya yake ikawa mbaya hadi akajitia kitanzi Alhamisi iliyopita.

Bi Wamuyu alisema marehemu alifanyiwa matibabu mengi katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nanyuki, Nyeri Hospice, Aga Khan, Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Meru na Hospitali ya Nairobi South.

“Hivi majuzi alikuwa akiniuliza kama upasuaji utakuwa na uchungu. Wakati mwingine alieleza matumaini yake na kusema anasubiri kwa hamu kufanyiwa upasuaji ili sehemu iliyofura tumboni mwake iondolewe kabisa,” akasema Bi Wamuyu.

Aliongeza: “Alikuwa akisisitiza kwamba jamaa zake walimsaidia sana kifedha na kihisia na Mungu angewatuza pakubwa.”

Dadake marehemu, Bi Grace Njeri, aliomba serikali ihakikishe gharama ya matibabu ya kansa imepunguzwa na vituo vya matibabu ya saratani vifunguliwe katika hospitali zote za umma.

“Kakangu alikuwa amemaliza rasilimali zake zote kwa matibabu lakini tulihakikisha bili zote za matibabu zililipwa kwa wakati uliofaa,” akasema Bi Njeri.

Alisema walikuwa wanatumia karibu Sh40,000 kila wiki kwa matibabu yake.

Kisa hicho kilitokea wiki moja tu baada ya mwanamke wa miaka 40 aliyeugua kansa ya matiti kujitoa uhai katika nyumba ya dadake mjini Naivasha.

Kumekuwa na ongezeko la visa vya kansa nchini.