Habari Mseto

Aliyekufa kwa corona azikwa bila utaratibu

April 12th, 2020 2 min read

Na DICKENS WASONGA

HUZUNI, hamaki na hali ya mshangao mkubwa ilikumba kijiji cha Kamalunga, eneo la Ukwala, Kaunti ya Siaya wakati maafisa wa serikali walipowasili usiku wa manane kumzika mwanamume aliyefariki kwa virusi vya corona.

Kifo cha James Oyugo Onyango, 59, kilifanya idadi ya waliofariki kwa virusi hivyo kuongezeka hadi wanane jana, huku maambukizi mapya sita yakitangazwa na kufikisha idadi kuwa 197.

Hii ni mara ya tatu nchini kwa maambukizi ya corona kubainika baada ya mgonjwa kufa, hali inayoibua maswali kuhusu usalama wa umma hasa kwa matibabu wanaoshughulikia wagonjwa wa kawaida.

Mwili wa marehemu ulichukuliwa na maafisa wa Wizara ya Afya na wengine wa usalama kutoka katika Hospitali ya Matibabu Foundation iliyo mjini Ukwala, ukazikwa mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia jana.

Kilio kilitanda nyumbani kwake wakati mwili huo uliofunikwa kwa mfuko wa maiti bila jeneza, ulipowasili kwa gari aina ya pick-up.

Maafisa waliovaa magwanda meupe ya kujikinga kutokana na viini ndio walioshughulikia mazishi hayo ambayo yalijumuisha tu kuondoa mwili katika gari, kuubeba hadi katika kaburi dogo na kuutupa ndani kisha kulifukia kwa mchanga.

Sauti za waliokuwa wakilia zilisikika zikisema kwa Kiluo: “Baba, hawafai kukuzika namna hii…” na mwingine akilia kwa hamaki, “Huo ni mwili wa nani mnaotupa namna hiyo…”

Desturi zote za mazishi zilitupwa kando, isipokuwa kwa jamaa mmoja pekee aliyewaelekeza maafisa hao kuhakikisha kuwa kichwa cha marehemu kimetazama upande uliofaa kaburini.

Jamaa za marehemu pamoja na wanakijiji wapatao 30 walichukuliwa mara moja na kupelekwa kutengwa katika Taasisi ya Mafunzo ya Matibabu ya Siaya, watakaposubiri kuthibitishwa ikiwa waliambukizwa virusi vya corona.

Ripoti ya polisi ilionyesha kuwa marehemu alikuwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) mjini Mombasa.

Kulingana na polisi, alikuwa ametoka Mombasa mnamo Aprili 5, akasafiri pamoja na mkewe na watoto wake wawili hadi bomani kwake Siaya.

Walilala Nairobi usiku mmoja kabla kuendeleza safari yao Aprili 6. Walipokuwa njiani, walipata ajali ndogo eneo la Awasi, barabara kuu ya Kericho-Kisumu lakini hakuna aliyejeruhiwa.

Gari hilo lilivutwa hadi katika Kituo cha Polisi cha Awasi, kisha kaka yake akamchukua pamoja na familia yake na kuwapeleka Kisumu.

Alilala Kisumu, kisha akawasili Ukwala mnamo Aprili 7 kwa gari la kakaye lakini hakutoka nje ya nyumba.

Mnamo Ijumaa, Aprili 10, alianza kukohoa mwendo wa saa nne asubuhi ambapo alikimbizwa hadi hospitali ya kibinafsi ya Matibabu Foundation kisha akafariki saa moja usiku huo.

Chembe zake za damu zilichukuliwa Jumamosi, Aprili 11 na kupelekwa katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini (KEMRI) mjini Kisumu, ndipo ikabainika alikuwa ameambukizwa virusi vya corona kabla ya kufariki.

Duru katika idara ya polisi zilisema, ilibidi mwili wake unyunyiziwe dawa na uzikwe mara moja ili kuzuia ueneaji wa viini.

Ilifichuka kuwa marehemu, ambaye ni mume wa wake wawili, alikuwa ameondoka nyumbani kwake Likoni, Kaunti ya Mombasa mnamo Aprili 5 kupitia kivukio cha Likoni.

Mbali na jamaa na wanakijiji, matabibu tisa wa Hospitali ya Matibabu pia walitengwa jana.