Habari Mseto

Aliyekuwa mkurugenzi wa Chase Bank arudisha paspoti

December 10th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

Wakili Cecil Miller Jumatano alirudisha mahakamani paspoti ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa benki iliyofilisika ya Chase Bank.

Bw Miller alisema Bw Mohammed Nazrullah Khan alisafiri hadi nchini Amerika kupokea matibabu ya moyo.

“Hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani alikuwa ameamuru Bw Khan arudishe kortini pasipoti yake akirudi kutoka Marekani,” Bw Miller alimweleza hakimu.

“Pasipoti niko nayo na Bi Onkwani hayuko kazini nimweleze hayo. Alikuwa ameamuru niirudishe leo Jumanne,” Bw Miller alimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Hata hivyo  kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Avedi aliomba mahakama ipokee pasipoti hiyo kwa niaba ya Bi Onkwani.

Zafrullah ameshtakiwa pamoja na waliokuwa wakuu katika benki hiyo Bw Duncan Kabui, James Mwaura na Makarios Omondi kwa ulaghai wa zaidi ya Sh1.6bilioni.