Aliyekuwa afisa wa mechi ya UEFA iliyotibuka kati ya PSG na Istanbul Basaksehir apigwa marufuku

Aliyekuwa afisa wa mechi ya UEFA iliyotibuka kati ya PSG na Istanbul Basaksehir apigwa marufuku

Na MASHIRIKA

REFA raia wa Romania, Sebastian Coltescu aliyekuwa mwamuzi msaidizi katika mechi ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha Paris Saint-Germain (PSG) na Istanbul Basaksehir ya Uturuki mnamo Disemba 8, 2020, sasa amepigwa marufuku hadi mwisho wa kampeni za msimu huu.

Afisa huyo wa mechi amepokezwa adhabu hiyo baada ya uchunguzi kubaini kwamba alidhihirisha “mienendo inayokiuka maadili ya uanaspoti mwema”.

Mchuano huo uliochezewa uwanjani Parc des Princes, Ufaransa, ulisitishwa na wasimamizi wa kipute cha UEFA baada ya Coltescu kutuhumiwa kutumia matamshi yaliyodhihirisha ubaguzi wa rangi dhidi ya Pierre Webo – kocha raia wa Cameroon ambaye kwa sasa ni mkufunzi msaidizi kambini mwa Basaksehir.

Hata hivyo, uchunguzi wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) ulibaini kwamba Coltescu hakuwa amekiuka kanuni zozote zinazodhibiti masuala ya ubaguzi wa rangi miongoni mwa wanasoka, mashabiki au wasimamizi wa vikosi kutoka mataifa wanachama wa shirikisho hilo.

Ingawa Octavian Sovre aliyekuwa pia refa msaidizi wa mechi hiyo iliyotibuka baada ya dakika 14 za kipindi cha kwanza alihojiwa na Uefa katika uchunguzi wao, hakupigwa marufuku wala kupokezwa adhabu yoyote. Coltescu alipatikana na hatia ya kukiuka sheria za Kifungu cha 11(1) na 6(1) kwenye kanuni za Uefa kuhusu nidhamu na atatakiwa sasa kuhudhuria mafunzo spesheli ya Uefa kuhusu lugha ya heshima na upole kufikia Juni 2021.

Webo ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Cameroon, alionyeshwa kadi nyekundu wakati wa mchuano huo kwa kuzozana na Coltescu pembezoni mwa uwanja.

Hatua hiyo ilichochea wachezaji wa Basaksehir kuondoka uwanjani wakilalamikia tukio hilo la ubaguzi wa rangi nao wakafuatwa na wanasoka wa PSG.

Tukio hilo lilifanyika katika dakika ya 14 ya mchezo, vikosi vyote viwili vikiwa bado havijafungana bao katika gozi hilo la Kundi H.

Mchuano huo hata hivyo uliendelezwa siku iliyofuata, yaani Disemba 9, 2020 uwanjani Parc des Princes na PSG wakaibuka na ushindi wa 5-1. Mechi hiyo ya marudiano iliongozwa na maafisa wapya – Danny Makkelie wa Uholanzi akisaidiana na Mario Diks wa Uholanzi pamoja na Marcin Boniek na Bartosch Frankowsky kutoka Poland.

Vikosi vingine vilivyokuwa katika Kundi hilo la H kwenye UEFA ni Manchester United ya Uingereza na RB Leipzig ya Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Pep aridhishwa na rekodi ya Man-City kwenye vita vya...

Ligi ya daraja la pili yapamba moto