Aliyekuwa meya Lamu ageuka bodaboda kujipatia riziki

Aliyekuwa meya Lamu ageuka bodaboda kujipatia riziki

Na KALUME KAZUNGU

HALI ngumu ya maisha imemsukuma aliyekuwa diwani na mwenyekiti wa baraza la mji wa Lamu, wadhifa ambao ni sawa na wa meya, Bw Abdulaziz Allan Kicheko kuwa mhudumu wa bodaboda.

Kila Bw Kicheko anapopita karibu na majengo ya bunge la kaunti eneo la Mokowe, yeye hukumbuka jinsi alivyokuwa akilakiwa kama mgeni wa heshima enzi zake za uongozi.

Jengo hilo zamani lilikuwa likitumiwa na madiwani aliokuwa akiongoza vikao vyao jinsi ambavyo spika wa bunge hufanya, lakini tangu katiba mpya ilipopitishwa 2010, huwa linatumiwa na wawakilishi wa wadi.

Anapozungumzia enzi hizo, yeye hueleza jinsi alivyokuwa akivalia joho leusi na ushanga wa dhahabu kuashiria mamlaka yake makubwa ila sasa, analazimika tu kuvalia mavazi ya kujisitiri na upepo mkali ilivyo kawaida ya bodaboda.

Baba huyo wa watoto sita aliye na umri wa miaka 54, analaumu serikali kuu kwa kutowajali madiwani wa zamani ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilalamika kupuuzwa licha ya mchango wao kwa taifa.

“Mpaka sasa, serikali bado ina deni langu. Kuna miezi mingi ambapo hatukulipwa mishahara lakini kila tunapoulizia, hakuna anayejitolea kutulipa. Hiyo ni sababu moja inayonifanya nisiwe na furaha kuhusu kazi niliyofanyia baraza la jimbo la Lamu,” akasema Bw Kicheko.

Alihudumu kwa vipindi viwili. Kwanza kama diwani maalumu kati ya 1997 hadi 2002, kisha akashinda uchaguzini na kuwa diwani wa Wadi ya Faza/Tchundwa kati ya 2002 na 2007.

Katika kipindi hicho cha pili ndipo alichaguliwa mwenyekiti wa baraza hilo, wadhifa ulio sawa na wa meya waliokuwa wakisimamia mabaraza ya manispaa.

Kitaifa, mameya ambao wangali wanavuma kwa uongozi ni kama vile Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala aliyekuwa Meya wa Mombasa, na Mbunge wa Kisumu Mashakiri Shakeel Shabbir aliyekuwa Meya wa Kisumu.

Bw Kicheko alisema alipokuwa akiondoka mamlakani, alikuwa amehifadhi pesa kidogo sana ambazo hazingetosha kugharamia mahitaji yake na familia yake kwa mwaka mmoja.

Alitafuta kazi zingine, akawa dereva wa aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Lamu, Bi Shakila Abdalla kati ya 2009 na 2013.

Kandarasi hiyo ilipokamilika, aliamua kuwa mvuvi lakini changamoto za sekta hiyo zikamlazimu kuwa mhudumu wa bodaboda.

“Ombi langu kwa wabunge ni watusaidie kushinikiza serikali itulipe kiinua mgongo na pensheni ya kila mwezi ili tujiendeleze kimaisha,” akasema.

You can share this post!

Auza nyumba ya babake akimdai Sh200,000

Diwani wa zamani kizimbani kwa mashtaka ya mauaji