Habari

Aliyekuwa mkurugenzi wa KVDA akamatwa

July 26th, 2019 1 min read

Na VINCENT ACHUKA

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Ustawishaji wa Kerio Valley (KVDA) David Kimosop amekamatwa na anahojiwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Kimosop amekamatwa Ijumaa asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) mara tu alipotua nchini akitokea jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia  Tanzania.

Ni miongoni mwa washukiwa wakuu katika sakata ya mabwawa ya Kimwarer na Arror ya Sh63 bilioni.

Washukiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich, aliyekuwa katibu Kamau Thugge, Susan Koech, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira (Nema) Geoffrey Wahungu. Walishtakiwa na kuachiliwa kwa dhamana Jumanne.

Wakati huo, wakili wa Kimosop ambaye ni Bw Katwa Kigen aliitaka mahakama kumpa muda zaidi kwa sababu “mteja wangu hayuko nchini.”

“David Kimosop yuko nchini DRC na alitarajiwa kuwasili Jumamosi,” Bw Kigen alisema.

Akaongeza: “Nimemshauri arejee mapema na amesema kufikia Alhamisi atakuwa amewasili. Ninaiomba mahakama iniruhusu nimwasilishe Ijumaa,” Kigen akasema wakati huo.