Habari Mseto

Aliyekuwa mtangazaji wa KTN akiri kuhadaa polisi

July 15th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

MTANGAZAJI wa zamani wa KTN, Bi Esther Arunga amekiri kwamba aliwadanganya polisi kuhusu kilichosababisha kifo cha mwanawe mnamo 2014 nchini Australia.

Mumewe Quincy Timberlake amekuwa akilaumiwa kwa kumuua mtoto huyo aliyekuwa wa miaka mitatu.

Kulingana na kiongozi wa mashtaka, Danny Boyle, Bi Arunga aliwaambia maafisa kuwa mtoto huyo alianguka kutoka chumba cha juu walimoishi.

Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi wa mwili huo ilibainisha kuwa mtoto huyo alifariki baada ya kufinywa kwa nguvu tumboni mwake lakini si kutokana na kuanguka.

Boyle alisema Bi Arunga alikaa siku 26 bila kueleza ukweli, lakini alifichua hayo baada ya mumewe kupelekwa kufanyiwa ukaguzi wa kiakili.

Alieleza kuwa siku ambayo mtoto huyo alifariki, alimkuta Timberlake akimpiga na kumgongesha kutani.

Awali, alikuwa amewaambia wachunguzi kuwa mumewe alifanya hivyo ili “kuondoa shetani” aliyeamini alikuwa tumboni mwake.

Boyle alisema ijapokuwa Bi Arunga hakuingilia ushahidi, alihusika kuwazuia wachunguzi kumkamata mshukiwa mkuu. Atahukumiwa Alhamisi.