Kimataifa

Aliyekuwa Rais wa Peru ajiua kukwepa mashtaka ya hongo

April 17th, 2019 2 min read

MASHIRIKA NA DANIEL OGETTA

RAIS wa zamani wa Peru, Alan García alijiua kwa kujipiga risasi Jumatano wakati maafisa wa polisi walipofika nyumbani kwake kumkamata kuhusiana na tuhuma za kumumunya hongo ya mabilioni ya pesa.

Bw García alikimbizwa hospitalini katika jiji kuu la Lima lakini akafariki saa chache baadaye. Kifo chake kimethibitishwa na rais wa sasa wa Peru Bw Martin Vizcarra.

Wafuasi wake walijumuika nje ya hospitali hiyo huku maafisa wa polisi wakipata wakati mgumu kuwadhibiti. Bw García alituhumiwa kumeza hongo kutoka kwa Odebrecht ambayo ni kampuni ya ujenzi ya Brazil, tuhuma alizozikana.

Maafisa walitumwa kumkamata kwa kuhusiana na tuhuma hizo za kula hongo, lakini akatumia hila na hatimaye kujiondoa uhai.

Waziri wa Maswala ya Ndani, Bw Carlos Morán aliambia wanahabari kwamba polisi walipowasili, Bw García aliomba kupewa fursa ya kupiga simu, kisha akaingia kwenye chumba kimoja na kuufunga mlango.

Dakika chache baadaye, mlio wa bunduki ulisikika, alieleza Bw Morán. Polisi walilazimika kuufungua mlango huo kwa fujo na kumpata García ameketi kitini akiwa na donda la risasi kichwani mwake.

García alifanyiwa upasuaji wa dharura katika hospitali ya Casimiro Ulloa lakini juhudi hizo hazikufua dafu.

Kwenye mtandao wake wa Twitter, Bw Vizcarra alisema kuwa “alipigwa na butwaa” kutokana na kifo cha rais huyo wa zamani n ahata kuwatumia risala za rambirambi jamaa za mwendazake.

García alihudumu kama rais kutoka 1985 hadi 1990 na kurejea tena mamlakani 2006 hadi 2011.

Makachero wanasema kwamba alipokea rushwa kutoka kwa kampuni ya Odebrecht alipokuwa akihudumu kwa mara ya pili kama rais.

Kampuni hiyo ya Odebrecht tayari inadaiwa kumlipa rais huyo wa zamani rushwa ya Sh3 bilioni tangu 2004.

Lakini Bw García amekana tuhuma hizo na kusema ni vita vya kisiasa tu. Jumanne kwenye akaunti yake ya Twitter, alisema kwamba hana habari zozote kuhusiana na madai hayo.

Muhtasari kumhusu Alan García

  •  Alizaliwa 23 Mei 1949 mjini Lima
  • Alisomea uanasheria na sosholojia
  • Alichaguliwa katika mahakama ya Peru kwa chama cha Peru (APRA)
  • Alikuwa rais wa mchanga zaidi wa Peru aliingia mamlakani mnamo 1985 akiwa na miak 36
  • Ni mlumbi hodari, wengine walimtaja kama “John Kennedy wa Amerika ya Kilatini”
  • Alihudumu kama rais kwa vipindi viwili, mara ya kwanza 1986-1990, kisha 2006-2011
  • Alikuwa anachunguzwa kwa tuhuma za kumeza rushwa katika sakata ya Odebrecht

Sakata ya Odebrecht

Odebrecht ni kampuni kuu ya ujenzi ya Kibrazili inayofahamika kwa kuunda miundomsingi na majengo tajika  duniani ikiwemo viwanja kadhaa vilivyotumika katika Olimpiki ya 2006 na hata dimba la Kombe la Dunia katika nchi hiyo.

Lakini, kampuni hiyo imekiri kwa makachero kuhusika katika utoaji wa mlungula kwa zaidi ya nusu ya nchi za Latini ya Amerika pamoaj na Angola na Msumbiji za Afrika.

Makachero wanasema kuwa Odebrecht ilihonga maafisa au wawaniaji viti mbalimbali katika siasa ili kupata kandarasi za ujenzi. Sakata hii imewapata viongozi wengi katika Amerika ya Kilatini.

Marais wanne wa Peru waliokuwa mamlakani, wanachunguzwa kwa tuhuma za kushirikiana na kampuni hiyo katika ulaji rushwa akiwamo wa nne Alberto Fujimori – anayehudumia kifungo chake kwa kukiuka haki za binadamu na ulaji rushwa.

Kiongozi wa zamani, Pedro Pablo Kuczynski alipelekwa hospitalini mnamo Jumatano siku kadhaa baada ya kukamatwa kwake kufutia uhusiano wake na sakata ya Odebrecht. Duru zinaarifu kwamba alipelekwa katika kitengo cha walio mahututi.

Kiongozi wa sasa wa upinzani, Keiko Fujimori, pia alikamatwa kwa tuhuma hizo hizo kwa kupokea pesa zinazokadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni kilaghai.

Mnamo Oktoba, kura za maoni zilionyesha kuwa asilimia 94 ya wananchi wa Peru waliamini kuwa kiwango cha rushwa kilikuwa juu katika nchi yao.