Habari za Kitaifa

Aliyekuwa Waziri Franklin Bett ajeruhiwa kwenye ajali Kericho


ALIYEKUWA Waziri wa Barabara Franklin Bett alipata majeraha baada ya kuhusika kwenye ajali katika barabara kuu ya Kericho-Kisumu Alhamisi usiku, Agosti 15, 2024.

Kulingana na ripoti ya polisi gari ambalo Waziri huyo wa zamani alikuwa akisafiria, liligonga trekta iliyokuwa ikisafirisha miwa.

Ajali hiyo ilitokea karibu na Karange katika eneo la Awasi-Kericho mwendo wa saa moja usiku.

“Kutokana na ajali hiyo, Bw Bett alipata jeraha sehemu ya mbele ya kichwa huku wanawake wengine wawili watu wazima na dereva wakipata majeraha madogo,” ripoti ya polisi inasema.

Bw Bett na abiria wengine waliokuwa kwenye gari hilo walikimbizwa katika hospitali ya Awasi Catholic wakiwa katika hali nzuri na baadaye wakapelekwa hospitali ya Aga Khan kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, duru katika familia yake zilisema Ijumaa asubuhi, Agosti 16, 2024 kwamba mwanasiasa huyo wa zamani alipelekwa katika hospitali ya Siloam katika mji wa Kericho.

“Waziri huyo wa zamani yuko katika hali nzuri na ataruhusiwa kuondoka leo kwa vile alilazwa usiku kucha kwa uchunguzi,” mtu wa familia ambaye hakutaka kutajwa jina aliambia Taifa Dijitali kwa njia ya simu.

Aliongeza, “Nimetoka kumuona hospitalini asubuhi ya leo na yuko sawa. Hakuna sababu ya kutisha.”

Gari ambalo mwanasiasa huyo alikuwa akisafiria baadaye lilivutwa hadi kituo cha polisi cha Awasi.

Polisi walieleza kuwa trekta lililohusika katika ajali hiyo halikusimama na linaendelea kutafutwa.

Kulikuwa na mvua kubwa wakati wa ajali hiyo kulingana na polisi.