Habari Mseto

Aliyemuua nyanyake na kuhepa asakwa

September 24th, 2018 1 min read

NA ALEX NJERU

MWANAMUME katika kijiji cha Kieranthi, eneo la Tharaka Kaskazini anatafutwa na polisi baada ya kudaiwa kumkatakata nyanyake Jumamosi jioni hadi akafariki.

Kulingana na Naibu Chifu wa eneo la Kamaguna, Bw John Nyaga Gakingo, mwanamume huyo Jeremiah Kirimi Mutiria alidaiwa kumvamia Bi Jenifer Kaguna kwa upanga akiwa nyumbani mwake na kumkata mara mbili shingoni.

Alisema nyanya huyo ambaye alijaribu kutoroka kutoka kwa mjukuu wake aliyemkimbiza kwa upanga alishambuliwa kwenye lango la boma yake ambapo alianguka na kufa.

“Nilipata mwili wa nyanya huyo umelowa damu kwenye lango la boma ambapo alikuwa ameanguka,” alisema Bw Gakingo.

Aliongeza kuwa baada ya kufanya uhalifu huo, mshukiwa alitoroka kuelekea soko la Kathangacini akitumia pikipiki huku wanakijiji wakitishia kumuadhibu.

Bw Gakingo alisema aliwaita polisi ambao walichukua mwili na kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Chuka huku uchunguzi ukianzishwa na mshukiwa akisakwa.

Alisema sababu ya shambulio hilo haijajulikana lakini wakazi walidai mwanamume huyo amekuwa akitisha kumuua nyanyake.

Wakazi waliwaambia wanahabari kwamba familia hiyo imekuwa na mgogoro wa kinyumbani kwa muda mrefu lakini hawakutarajia tukio kama hilo.

“Hata kama wawili hao wamekuwa na mgogoro, hatukutarajia kuwa jambo kama hilo lingetokea,” alisema Bi Muthoni.