Habari Mseto

Aliyemwekea dhamana kinara wa KEBS aliyekufa aitwa kortini

June 20th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MKENYA aliyemwekea dhamana Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS) wa zamani, Dkt Kioko Mang’eli, aliyefariki, atahitajika kortini Julai 28 ili kutamatisha kesi dhidi ya mwendazake.

Bw Mang’eli alikabiliwa na shtaka la kuunganisha umeme kinyume cha sheria mtaani Karen, Nairobi.

Upande wa mashtaka uliambia Hakimu Mkuu wa Kibera kwamba polisi walimfahamisha kuwa Dkt Mang’eli aliaga dunia mapema 2019 na kwa hivyo kesi haiwezi kuendelea.

“Nimepata habari kwamba mshtakiwa aliaga dunia japo kulikuwa na kibali cha kumkamata kwa kukosa kufika kortini. Kutokana na hali hii, kesi haiwezi kuendelea,” Kiongozi wa mashtaka Bi Zafida Chege alieleza mahakama.

“Ninaomba mahakama imuite mtu aliyemsimia dhamana ili aweze kuwasilisha cheti za kuonyesha mshtakiwa aliaga dunia. Hii ni muhimu kabla ya kesi kuondolewa,” alisema Bi Chege.

Dkt Mang’eli alitoweka baada ya kuachiliwa kwa dhamana katika kesi aliyoshtakiwa kwa kuunganisha stima kinyume cha sheria katika makazi yake mtaani Karen mnamo Juni 25 2017.

Ilidaiwa kwamba kampuni hiyo ilikuwa imekata stima ikimdai zaidi ya Sh600,000. Hata hivyo, badala ya kulipa alivyotakiwa aliunganisha stima tena na kuendelea kutumia hadi maafisa wa kampuni hiyo walipompata na kumkamata.

Alimwachilia Bw Mang’eli kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu lakini hakufika kortini wala kutuma wakili wa kumwakilisha. Dhamana yake ilitwaliwa na serikali 2018 na polisi wakaagizwa wamsake na kumkamata wamfikishe kortini.

Hata hivyo hawakuweza kumkamata hadi Alhamisi mahakama ilipofahamishwa aliugua na kuaga dunia.

Kesi hiyo itatajwa Julai 28 ili aliyemwekea dhamana awasilishe cheti kuthibitisha kifo chake kabla ya kesi kuondolewa rasmi