Habari Mseto

Aliyenaswa na pingu akiwa mlevi asukumwa rumande

June 12th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KIBARUA aliyejikanganya mbele ya mahakama aliposhtakiwa kupatikana na pingu kinyume cha sheria Jumatano alisukumwa gerezani na kesi inayomkabili kuorodheshwa kusikizwa Juni 28, 2018.

Peter Irungu Wanjiku aliyeshtakiwa Jumanne mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi alijikanganya na kuamriwa afikishwe mbele ya hakimu mkazi Bw Paul Mayova kueleza ikiwa alipatikana na pingu zilizoibwa kutoka kwa idara ya polisi.

Jumatano , alipofikishwa mbele ya Bw Mayavo, Irungu alirejelea msimamo wake wa Jumanne kwamba aliziokota pingu hizo na kamwe “hakujua zimeibwa.”

Akijibu shtaka mbele ya Bw Mayavo , mshtakiwa alisema, “Mimi nilikuwa mlevi nilipookota pingu hizo. Niliwaonyesha wenzangu tuliokuwa tunabugia pombe na nikawaambia nitazipeleka katika kituo cha Polisi cha Kilimani. Nilikamatwa na maafisa wawili wa Polisi wa Utawale kabla ya kufika Kilimani.”

Baada ya kusimulia hayo , Bw Mayavo alimweleza , “Hii mahakama imesajili kwamba umekanusha shtaka kwa vile umesema uliziokota pingu hizo.”

Kiongozi wa mashtaka Edna Ntabo akikagua faili. Picha/ Richard Munguti

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh10,000 na kurodhesha kesi dhidi ya mshtakiwa isikizwe kuanzia Juni 28, 2019.

Shtaka dhidi ya Irungu lilisema katika soko la Kenyatta Market karibu na mtaa wa mabanda wa Kibera alipatikana akiwa na Pingu mali ya idara ya Polisi.

Alipofika mbele ya Bw Andayi , mshtakiwa alisomewa shtaka kisha akaulizwa “ni kweli ama sio kweli.”

“Je, unajua pingu ulizokamatwa nazo zimeibwa,” hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

“Mimi nilikamatwa Juni 7, 2019 na polisi nikipeleka pingu hizo katika kituo cha Kilimani.Sikuziiba pingu hizo. Niliziokota nikiwa na marafiki wengina katika mtaa wa Ngumo,” Peter Irungu alimjibu hakimu.

Pingu alizopeleka katika kituo cha polisi. Picha/ Richard Munguti

“Nimekuuliza ikiwa ulijua pingu hizo zilikuwa zimeibwa,” Bw Andayi akamwuliza tena.

“Nami nimekuambia nilikuwa napeleka pingu kituo cha polisi cha Kilimani nilipotiwa nguvuni. Sijui kama zilikuwa zimeibwa ila niliziokota,” mshtakiwa alimjibu.

Mshtakiwa alikiri alipatikana na pingu hizo na kuomba mahakama imsamehe kwa vile hakujua pingu zimeibwa.

Hakuweza kulipa dhamana na hivyo akausumwa rumande huku akilia mke wake na mtoto watataabika.