Aliyening’inia kwa ndege kushtakiwa leo Jumatatu kwa jaribio la kujitoa uhai

Aliyening’inia kwa ndege kushtakiwa leo Jumatatu kwa jaribio la kujitoa uhai

NA GITONGA MARETE

MWANAUME ambaye alining’inia kwenye helikopta ambayo ilimbeba Waziri wa Kilimo Peter Munya mnamo Jumatano, atashtakiwa kortini leo Jumatatu kutokana na jaribio la kujiua.

Bw John Mutwiri,41 aliwasilishwa katika Mahakama ya Maua mnamo Alhamisi wiki jana, lakini hakushtakiwa baada ya mama yake kueleza mahakama kuwa alikuwa na tatizo la kiakili.

Mahakama ilimtaka mama yake awasilishe stakabadhi ambazo zinathibitisha kuwa Bw Mutwiri alikuwa na akili taahira.

Pia imebainika kuwa Bw Mutwiri aliruka kutoka ghorofa ya kwanza ya jengo moja jijini Nairobi miaka michache iliyopita na kupata majeraha madogo.

Mkuu wa Polisi wa Igembe Kusini Hussein Ali, alieleza Taifa Leo kuwa walimkamata Bw Mutwiri mnamo Alhamisi, akahojiwa na akasema alitaka kusafiri kuelekea Nairobi kama sababu ya kuning’inia kwenye helikopta hiyo.

“Tulitaka kujua kwa nini alining’inia kwenye helikopta na akasema lengo lake lilikuwa kufika Nairobi ili kusaka ajira,” akasema Bw Ali kupitia mazungumzo ya simu na Taifa Leo.

Bw Muturi alizua taharuki na hofu katika soko la Kiegoi, Meru eneobunge la Igembe Kusini mnamo Jumatano kwa kuning’inia kwa ndege hiyo wakati ambapo Bw Munya na Mbunge wa EALA Mpuru Aburi, walikuwa wakiondoka baada ya kuhutubia mkutano wa kisiasa.

Ndege hiyo ilipoanza kupaa angani, wakazi waligundua kuwa kulikuwa na mwanaume ambaye alikalia na kukwamilia chuma katika upande ambao ndege hutumia kutua. Wakazi hao walimwaashiria rubani asiendelee kupaa angani zaidi ili Bw Mutwiri ashuke lakini jamaa huyo alikataa.

Wakati wa kisa hicho, Bw Aburi alionekana dirishani akijaribu kuwaeleza baadhi ya wakazi waliokuwa wakimshangilia mwanaume huyo jambo fulani.

Muda huo wote, Bw Mutwiri hakuonekana kutatarika huku akipungia umati mkono. Baada ya rubani kulazimika kutua, alitimka mbio na kuwazidi maarifa maafisa wa polisi huku wakazi nao wakiwataka maafisa hao wa usalama wasimdhuru kwa kichapo. Alitoweka kabla ya kukamatwa baadaye Alhamisi.

Hata hivyo, hiki si kisa cha kwanza cha mtu kuning’nia kwenye helikopta katika Kaunti ya Meru. Mnamo 2017, Julius Mwathilie kutoka kaunti hiyo ambaye alitundikwa jina la utani ‘James Bond’, alining’nia kwenye ndege iliyokuwa imembeba Raila Odinga.

Bw Odinga alikuwa ameongoza mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Maili Tisa katika eneobunge la Igembe ya Kati ili kuwahimiza raia wajiandikishe kama wapigakura.

Rubani wa Bw Odinga alilazimika kutua katika Shule ya Msingi ya Muriri, katika eneobunge la Tigania Mashariki ambayo ni umbali wa kilomita 20.

Kama tu Bw Mutwiri, Bw Mwithalie alishtakiwa kwa jaribio la kujiua ila Bw Odinga aliingilia kati na akawaachiliwa huru.

  • Tags

You can share this post!

ODM yalaumiwa kuhusu uongozi wa Joho, Kingi

WANTO WARUI: Serikali ifanye ukaguzi wa kina wa majengo na...

T L