Habari MsetoSiasa

Aliyenuia kumuua Rais Ikulu amuomba msamaha

July 3rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa chuo kikuu aliyeingia Ikulu ya Nairobi kwa kuruka ukuta akiwa na lengo la kumuua Rais Uhuru Kenyetta Jumatano alimuomba msamaha Rais pamoja na Wakenya.

“Namuomba Rais Kenyatta na Wakenya msamaha. Sitarudia kosa hilo tena. Sitarudi kuchukua sheria mkononi mwangu tena. Nimepata funzo,” alisema Brian Bera Kibet.

Kibet aliyefikishwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Francis Andayi kujibu mashtaka ya kujiandaa kutekeleza uhalifu na kuingia Ikulu bila idhini aliomba asamehewe na mahakama kisha akubaliwe kurejelea maisha yake ya kawaida.

Baba yake mshukiwa huyo, David Kibet Maiyo, aliiomba korti imkabidhi mwanawe ampeleke hospitali.

Bw Maiyo alisema, “Alipoanza kuugua nilimpeleka hospitali ya Moi mjini Eldoret alikotibiwa na kupata afueni hata akarudi chuoni.”

“Je, uligudua mwanao ni mgonjwa lini? Na unataka hii mahakama ifanye nini?” Bw Andayi alimwuliza Mzee Maiyo.

“Niligudua Bera ni mgonjwa alipotoka nyumbani kwa miguu hadi eneo la Ortum kaunti ya Turkana. Alirudi akatembea tena kutoka JKUAT Ruiru hadi Mlima Kenya ndipo alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Naromoru,” alisema Maiyo.

Aliongeza kuwa mwanawe pia alitembea kwa siku nne kwa miguu kutoka Kitale hadi mjini Athi River, Kaunti ya Machakos.

Maiyo aliiomba mahakama imkabidhi mwanawe ampeleke kutibiwa aidha katika hospitali ya Moi ama Mathari.

Hakimu aliamuru mshukiwa huyo azuiliwe katika kituo cha Kilimani hadi Alhamisi atakapoamua ikiwa atamkabidhi baba yake au ataagiza apelekwe hospitali ya Mathari kupokea matibabu kisha arudishwe kortini kujibu mashtaka.

Bera alipigwa risasi begani alipoingia Ikulu akiwa amejihami kwa kisu. Aliondolewa na kupelekwa Hospitali Kuu ya Kenyatta alipolazwa kutibiwa.