Habari Mseto

Aliyenusurika Westgate 2014 aponea chupuchupu Dusit D2

January 16th, 2019 2 min read

VALENTINE OBARA NA NYABOGA KIAGE

BAADA ya milio ya risasi na vilipuzi kuzima katika kituo cha 14 Riverside ambako kuna Hoteli ya DusitD2 iliyoshambuliwa na magaidi Jumanne, mbivu na mbichi zimeanza kujulikana kuhusu waathiriwa na manusura.

Kwa Bi Tracy Wanjiru, 28, shambulio la Jumanne lilikuwa la pili la kigaidi kumpata kwani alikuwa ameponea shambulio la Westgate miaka sita iliyopita.

Wakati magaidi wa kundi haramu la al-Shabaab walipovamia Westgate mnamo Septemba 2013, Bi Wanjiru alikuwa mja mzito wa miezi sita na alikuwa kazini.

“Nilikuwa nafanya kazi hapo wakati magaidi walipovamia. Ilikuwa hali ngumu sawa tu na ilivyokuwa wakati huu. Kile ninachoweza kusema tu ni kwamba namshukuru Mungu,” akaeleza kwenye mahojiano ya kipekee.

Katika shambulio la DusitD2, Bi Wanjiru alikuwa karibu mno na washambuliaji kwenye saluni anayosimamia.

Alisema tukio la Westgate lilikuwa limemfunza kuhusu jinsi unavyoweza kujiokoa kwa kuitisha usaidizi kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini raia wa Marekani, Jason Spindler hakubahatika kwani alifariki katika shambulio hilo baada ya kuponea shambulio la kigaidi lililofanywa Septemba 11, 2001 na magaidi wa kundi la al-Qaeda nchini Amerika.

Bw Spindler alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la I-DEV International lenye afisi zake katika 14 Riverside.

“Ninasikitika kusema kuwa kakangu, Jason Spindler alifariki asubuhi hii wakati wa shambulio la kigaidi Nairobi, Kenya. Jason alinusurika wakati wa shambulio la 9/11 na alikuwa jasiri. Nina hakika alipambana nao vilivyo!” kakake, Jonathan Spindler, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Kwa familia ya Bw James Oduor, almaarufu kama Cobra, kifo chake katika mkasa huo wa Jumanne kilikuwa cha kusikitisha hasa kwa vile angesherehekea siku yake ya kuzaliwa jana.

Mamake, Bi Margaret Aluoch, alimtaja Bw Oduor, 28, kuwa mtu ambaye alipenda sana kandanda. Alikuwa akifanya kazi katika kampuni iliyo na afisi zake ndani ya 14 Riverside.

“Alipigwa risasi kifuani. Tulichoweza kujionea ni kwamba alivuja damu nyingi lakini tunasubiri upasuaji wa mwili wake ili kubainisha chanzo halisi cha kifo chake,” akasema Bi Aluoch alipohojiwa nje ya hifadhi ya maiti ya Chiromo, Nairobi..

Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed alisema binamu yake na rafikiye waliuawa kwenye shambulio hilo.

Binti ya aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale na mwanawe Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi na mwingine wa Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Vihiga, Bi Beatrice Adagala, walikuwa miongoni mwa manusura zaidi ya 700.