Habari Mseto

Aliyepaka polisi kinyesi na kutoroka anaswa

December 2nd, 2020 1 min read

Na STEPHEN ODUOR

POLISI katika eneobunge la Bura wamemkamata mahabusu aliyetoroka jela baada ya kumpaka kinyesi afisa wa polisi aliyempeleka kujisaidia haja msalani.

Abdul Awadh, 19, alikamatwa akielekea eneo la Nanighi takriban kilomita 30 kutoka Bura, huku akitumia kichochoro kuwatoroka polisi.

Kulingana na afisa msimamizi wa kituo cha Bura, Benedict Mwangangi, Bw Awadh alikuwa amezuiliwa kizuizini kwa kosa la kushambulia na kusababisha majeraha kwa mlalamishi kabla ya kutoroka kwake.

“Alipaswa kufikishwa mahakamani Desemba 10, hivyo tulikuwa tumemzuia huku tukiendelea na uchunguzi,” alisema.

Akiwa kizuizini saa moja alfajiri, Awadh aliomba ruhusa kwenda haja msalani,ambapo alisindikizwa na afisa wa zamu Antony Wanjau.

Hata hivyo alichukua muda mwingi sana msalani jambo lililomtia mlinzi wake wasiwasi na hivyo kumwamuru kutoka. Ndipo anadaiwa kumwagia mkorogo wa kinyesi usoni afisa yule na kutoroka.