Habari Mseto

Aliyepata 'A' katika KCSE afanya kazi gereji kwa kukosa karo

February 24th, 2019 2 min read

Na FRANCIS MUREITHI

KIJANA aliyepata alama ya ‘A’ yenye pointi 81 katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) mwaka wa 2015, amelazimika kufanya kazi katika gereji kwa kukosa karo ya kuendeleza masomo yake ya chuo kikuu.

Moses Oduor, 22, alitoka kwao katika kijiji cha Anduro, eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya kufanya kazi ya gerejii katika soko la Kabazi, eneobunge la Subukia, Kaunti ya Nakuru.

Alifanya KCSE katika Shule ya Upili ya Sawagongo iliyo Kaunti ya Siaya, ambapo alipata alama ya ‘A’ katika masomo sita ambayo ni Hesabu, Biolojia, Fizikia, Kemia, Historia na Jiografia huku akipata ‘A-‘ katika somo la Kiswahili na ‘B+’ katika Kiingereza.

Kwenye mkoba wake ambao hubebea vyeti vyake vya elimu, kuna pia vyeti viwili vya vifo vya wazazi wake, cheti cha kuzaliwa kwake na barua ya kujitambulisha iliyoandikwa na Naibu Chifu Joseph Aloo wa Lokesheni Ndogo ya Nyandiwa, kuthibitisha kwamba yeye ni yatima anayehitaji msaada.

“Watu wengi hushangaa wanapoona matokeo yangu mazuri na kujiuliza wazazi wangu waliko. Ninapowaambia mimi ni yatima huwa bado hawaamini ndiposa mimi hubeba vyeti hivi pamoja na vyangu vya elimu ili kuthibitisha hali yangu,” akaeleza Bw Oduor.

Alisema babake alifariki wakati alipokuwa katika darasa la nne mnamo 2007 na mamake akafa mwaka wa 2009 alipokuwa darasa la sita, hivyo basi akalelewa na nyanyake, Bi Monica Achieng’.

“Watu wengi ambao huja katika gereji hii hunihurumia na kutoa nakala za stakabadhi zangu na kuchukua nambari zangu za simu, wakiahidi kunisaidia kutimiza maazimio yangu ya kusomea masuala ya ndege. Lakini hakuna mabadiliko yametokea tangu nilipokuja katika gereji hii Juni mwaka uliopita,” akaeleza.

Yeye hupata malipo ya kati ya Sh50 na Sh200 kwa siku kwa kusugua magari yanayohitaji kupakwa rangi upya.

Alifichua kwamba alipata mwaliko kwa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta kusomea udaktari na upasuaji lakini hangeweza kugharamia masomo hayo.

Bw Joseph Waithaka, ambaye alifahamu kumhusu Bw Oduor wakati alipopeleka gari lake kutengenezwa, alisema masaibu yake yanasikitisha na haifai serikali kuacha vijana kama hao kuteseka.