Habari Mseto

Aliyeshtakiwa kumtusi Matiang'i akabiliwa na shtaka la kughushi kitambulisho

March 14th, 2018 1 min read

Wyclife Asuga Nyaega akiwa kortini Machi 13, 2018. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

AFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Jumanne ilitamatisha kesi dhidi ya kibarua aliyeshtakiwa kutuma jumbe za matusi kwa Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i.

Hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani alifutilia mbali ombi la kumchunguza Wyclife Asuga Nyaega na kuamuru apelekwe katika mahakama ya Kiambu kujibu mashtaka mengine ambayo korti haikufahamishwa.

Mawakili Okong’o Omogen na Ben Momanyi walisema mteja wao alifunguliwa kesi nyingine mbele ya hakimu mkuu Bw Francis  Andayi.

Bw Omogen alisema mshtakiwa pia alitakiwa kufika katika mahakama ya Kiambujana  saa nane kujibu mashtaka mengine.

Mawakili hao wawili walimuomba Bi Onkwani afutilie mbali ombi la kumfungulia mshtakiwa kesi ya kumdhihaki Dkt Matiang’i.

“Kwa vile mshtakiwa amefunguliwa mashtaka mengine naomba hii kesi uitamatishe. Polisi wako hapa wanataka kumpeleka Bw Nyaega Kitui,” alisema Bw Omogen.

Mbele ya Bw Andayi mawakili hao walisema kesi inayomkabili mshtakiwa ni ya kughushi kitambulisho na wala sio ya kumtusi waziri wa usalama.

“Tunaomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana,” aliomba Bw Omogen.

Lakini kiongozi wa mashtaka aliomba mshtakiwa akiachiliwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Parklands na hatimaye kupelekwa mahakama ya Kiambu kushtakiwa kwa kosa linginge.

“Tunaomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo kiwango cha juu. Tunataka kumpeleka mahakama ya Kiambu kujibu shtaka ambalo hatujui,” alisema Bw Omogen.

Mahakama ilimwachilia Bw Nyaega kwa dhamana ya pesa tasilimu ya Sh50,000.

“Kabla ya kupelekwa mahakama ya Kiambu mshtakiwa atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Parklands. Akilipa dhamana hiyo ataachiliwa kisha ajisalamishe katika korti ya Kiambu,” Bw Andayi alisema.

Bw Nyaega alishtakiwa kwa kughushi kitambulisho cha Bw William Muthusi na kufungua akaunti ya Mpesa akikitumia.

Kesi iliorodheshwa kusikizwa Aprili 9, 2018.