Habari Mseto

Aliyeshtakiwa kuuma mamake afunguka alikuwa anamchukia

February 18th, 2019 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

Mwanamke aliyeshtakiwa kwa kumuua mama aliyemzaa na kumlea miaka mitano iliyopita alikiri kwamba alikuwa akimchukia mama huyo.

Mahakama ya Nyeri iliamua kwamba Njoki Gachinga, 33, anafaa kujitetea katika kesi aliyoshtakiwa kwa kumuua Esther Wangari Kanuri mama aliyemuasili na kumlea alipotupwa na mama yake mzazi.

Mwili wa Bi Kanuri ulipatikana nyumbani kwake Kahuyo, Nyeri, Februari 23 2014 ukiwa umefungiwa chumba cha kulala cha Njoki.

Inadaiwa kwamba Njoki alimshambulia mama yake mlezi kwa kisu na kumdunga zaidi ya mara kumi na tano shingoni, kifuani na tumboni kisha akauvuta mwili kutoka sebuleni na kuufungia chumba chake cha kulala na kutorokea mjini Nyeri.? Ingawa alikanusha kwamba alimuua mama yake mlezi, mahakama iliamua kwamba ana kesi ya kujibu.

Akijitetea, mwanamke huyo ambaye ni mama ya mtoto mmoja, alikiri kwamba alikuwa akimchukia mama yake mlezi. Aliambia mahakama kwamba alikuwa akimtesa alipogundua kwamba hakuwa mama yake mzazi.? Akijitetea mbele ya Jaji Abigail Mshila, Njoki alikiri kwamba alikuwa mtundu tangu akiwa shule ya upili alipokuwa akivuta bangi. Alisema alianza kumkaidi mama yake mlezi baada ya kumaliza shule ya msingi 2001.

Alikiri kwamba alikuwa akimchukia sana marehemu kwa sababu ambazo hakufichua lakini akasema hakuwa na ubaya naye.? Kulingana na upande wa mashtaka, Njoki alimuua mama yake mlezi walipogombana akimtaka abadilishe tabia. Inasemekana alikasirika marehemu alipomuuliza kwa nini hakuwa ameenda kazini mjini Nyeri.

Njoki aliungama kuwa japo marehemu alikuwa akimwambia arekebishe tabia hakufuata ushauri wake.

Alisema alikuwa mtundu na alikuwa akimsumbua marehemu kwa tabia yake ya kutumia dawa za kulevya.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba hata akiwa shule ya upili, mshtakiwa alimwandikia barua baba yake mlezi Michael Kanuri kuomba msamaha kwa kumchukia marehemu.

“Kumbuka nilikuandikia arafa kukueleza nilikuwa nikimchukia mama. Ninatamani kumjua mama yangu mzazi,” inaeleza barua hiyo.? Mahakama iliambiwa kwamba siku mbili kabla ya siku anayodaiwa kumuua mama huyo, mshtakiwa alimweleza pasta wake, George Gichure Mwangi, kwamba angeua mtu.

“Sasa ninataka kuwa na pepo ninayojua kuliko malaika feki…wazazi wasio na shukrani…. Nitafanya maisha ya wazazi wangu kuwa jehanamu hapa duniani. Mapepo yaliyo ndani yangu yamekasirika na hayawezi kutulizwa.. nitaua yeyote atakayenikasirisha,” ulisema ujumbe aliomtumia pasta. Kesi itaendelea kusikilizwa Machi 27 2019.