Habari Mseto

Aliyetandika babake aambia korti kuwa yeye ni wazimu

March 29th, 2018 1 min read

Na TOTUS OMINDE

KULIKUWA na kicheko mahakamani Eldoret wakati mwanamume ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kumpiga na kumjeruhi babake kudai kuwa yeye ni kichaa. 

Mwanaume huyo aliambia mahakama kuwa alimpiga babake baada ya viwango vyake vya wazimu kupanda.

Isaac Kipruto Mutai ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kumpiga na kumjeruhi babake aliambia mahakama kuwa akili yake si timamu ambapo alikuwa akitumia dawa ya kupunguza makali ya matatizo ya kiakili.

Huku akiongea Kiingereza kwa ufasaha alionya, kuwa iwapo atazuiliwa rumande atasababisha uharibifu mkubwa  endapo viwango vya wazimu vitapanda.

Mutai alikuwa akijitetea mbele ya msajili wa mahakama mjini Eldoret Bi Mildred Munyekenye.

Alipoulizwa na msajili wa mahakama ni vipi alijua kuwa ana akili isiyo timamu, alisema anajifahamu vyema kuliko mtu mwengine yeyote.

“Mheshimiwa usipumbazwe na ufasaha wangu wa Kiingereza. Mimi ni wazimu. Naweza nikabadilika wakati wowote na kusababsiha uharibifu hata hapa mahakamani,” alisema mshtakiwa.

Mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alivamia babake mnamo tarehe 23 katika kijiji cha Segero Eldoret Magharibi ambapo alimsababishia majeraha.

Vile vile alikabiliwa na shtaka jingine la kujaza shimo la choo ambacho babake alikuwa amekodisha vijana kumchimbia ambacho kilikadiriwa kugharimu kima cha shilingi 5,000.  Alikiri mashtaka yote.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Aprili 16 baada ya mahakama kupokea ripoti kutoka kwa idara kifungu cha nje ili kubaini aina ya kifungo ambacho atafungwa.