Aliyetishia kumuua mpenziwe ahukumiwa

Aliyetishia kumuua mpenziwe ahukumiwa

Na KNA

MWANAMUME aliyetishia kumuua mpenzi wake wa zamani kutokana na deni la nyanya amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.

Mshtakiwa, aliyetambuliwa kama William Cheptumo, alipewa hukumu hiyo Ijumaa na mahakama moja ya Kabarnet, Kaunti ya Baringo.Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Bi Vienna Amboko, alisema baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa, mahakama ilimpata mshtakiwa akiwa na hatia.

Hukumu yake itajumuisha kufanya kazi ya jamii katika Shule ya Upili ya Kutwa ya Kilingot chini ya usimamizi wa mwalimu mkuu wa shule hiyo na mzee wa kijiji wa eneo hilo.Anadaiwa kufanya kosa hilo mnamo Januari 21 mwaka huu katika kijiji cha Kingoi, Kaunti Ndogo ya Baringo Kaskazini.

Hakimu alisema kuwa kulingana na mapendekezo yaliyowasilishwa mahakamani, aliona ikiwa heri kumpa mshtakiwa kifungo cha nje badala ya gerezani.Vile vile, aliagiza mshtakiwa kufanyiwa ukaguzi kuhusu matumizi ya mihadarati na kupewa ushauri maalum.

Mlalamishi, aliyetambuliwa kama Lydia Chepkwony, aliiambia mahakama kuwa wakati wa tukio hilo, alikuwa dukani mwake akiendelea na shughuli zake kama kawaida.Hata hivyo, mwendo wa saa moja unusu jioni, mshtakiwa alifika na kumwambia kumuuzia nyanya.

Alipomwitisha pesa, alikataa kulipa.Kulingana na mlalamishi, mshtakiwa aliingia kwa nguvu katika duka lake ambapo alichukua kisu na kujaribu kumdunga.Aliiambia mahakama kuwa aliokolewa na kakake, aliyekuwa nje ya duka hilo baada ya kufanikiwa kumnyang’anya kisu hicho.

  • Tags

You can share this post!

Uchaguzi wafanyika kundi maarufu likisusia

Copa America kung’oa nanga leo usiku