Aliyetumia wilbaro kama jukwaa ni MCA

Aliyetumia wilbaro kama jukwaa ni MCA

NA SIAGO CECE

TAKRIBAN miezi mitatu iliyopita, Bw Omar Mwaduga alikuwa mkazi wa kawaida kijijini Mshiu, Kaunti ya Kwale, akitafuta kiti cha udiwani.

Alianza kujulikana kitaifa wakati video yake ilisambazwa mitandaoni akihutubia wakazi katika mkutano wa muungano wa Kenya Kwanza, akiwa juu ya wilbaro iliyobebwa na vijana badala ya kutumia jukwaa.

Mkutano huo ulikuwa umehudhuriwa na Rais Mteule Dkt William Ruto.

Kulingana naye, alikuwa ashatumia rasilimali zote kufanya kampeni ikiwemo kuuza ng’ombe wake ili kupata fedha za mikutano na kuhamasisha wapiga kura kusikiliza sera zake.Wake zake wawili pia walikuwa wamechukua mikopo ya vyama vya akinamama ili kufadhili azma yake ya kisiasa.

Kufikia mapema Juni, Bw Mwaduga alikuwa bado hajakata tamaa kuwa diwani wa wadi ya Pongwe-Kikoneni katika kata ndogo ya Lungalunga, huku akitegemea majirani na wahisani kumchangia pesa za kampeni.

Lakini leo Bw Mwaduga ana furaha baada ya kuwashinda wapinzani na kutwaa kiti hicho.

Alizoa kura 2,982 mbele ya Renge Hassan (2,239) na Mguta Nasoro (1,548).

“Nimefurahi sana; yote ilikuwa kazi ya Mungu. Ushindi huu ni thibitisho kwamba watu niliowaamini hawakunikatisha tamaa,” diwani huyo mteule alieleza Taifa Leo.

Bw Omar Mwaduga alikuwa mkazi wa kawaida kijijini Mshiu, Kaunti ya Kwale, akitafuta kiti cha udiwani ambapo aliwahutubia wakazi akiwa juu ya wilbaro iliyobebwa na vijana badala ya kutumia jukwaa. PICHA | SIAGO CECE

Akiwa na umri wa miaka 34, Bw Mwaduga anatarajiwa kuwa miongoni mwa madiwani vijana katika Kaunti ya Kwale.

Kabla ya kuingilia siasa alikuwa mfanyabiashara wa makaa, ambayo ina faida kubwa mno Kwale.

Baada ya hapo alikuwa mwanaharakati huku akitumia magari yake kusaidia wanakijiji kupata huduma katika ofisi za serikali mjini Lungalunga.

“Wananchi ndio walinishawishi niingie siasa baada ya kuona jinsi nilivyowasaidia. Nafurahi wamenichagua,” Bw Mwaduga alisema.

Miongoni mwa masuala kipaumbele ni kufufua biashara ya makaa ambayo imepigwa marufuku huko na kuathiri wenyeji wengi.

Anapanga kuwasilisha swala hilo katika Bunge la Kaunti ya Kwale mara tu atakapoapishwa.

Bw Mwaduga pia anasema atasaidia wanafunzi wasiojiweza kupata ufadhili wa elimu pamoja na kupanua nafasi za ajira kwa vijana na wanawake.

“Maono yangu yanaenda sambamba na Dkt Ruto. Kwa mtazamo wake wa kiuchumi, nina hakika kwamba hii itahakikisha kila mmoja wa watu wangu ananufaika na huduma za serikali na kuboresha maisha yake,” akasema.

Aliongeza kuwa atafanya kazi kuhakikisha vijana waliojitolea muda wao kumfanyia kampeni wanathaminiwa vyema.

  • Tags

You can share this post!

USHAURI NASAHA: Endeleza jitihada za kujikuza, japo kwa...

Azimio wasisitiza kuwa mapambano yataendelea

T L