Kimataifa

Aliyevunja nyumba avute bangi ashtuka kupata simba ndani

February 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME aliyevunja na kuingia katika nyumba moja kuu kuu eneo la Texas, Marekani ili akavutie bangi humo ndani alishtuka, alipoingia na kupata simba marara akiwa amefungiwa humo ndani.

Mwanamume huyo anasemekana kupigia simu asasi za usalama kuzijulisha kuwa alikuwa amekutana na hatari, japo akisema kuwa mwanzoni alisema kuwa alidhani ni ndoto za bangi alipoona ‘paka mkubwa’.

Kisa hicho kilimfanya kutoka mbio ajabu baada ya kuona alikuwa amekumbana na kifo, akienda kuitisha msaada.

Maafisa wa kushughulika na maslahi ya wanyama walisema walimpata Simba Marara huyo Jumatatu na kuwaita polisi ili kusaidiana kumwondoa mnyama huyo humo ndani.

“Ni kama nyumba hii imefanywa mbuga ya aina fulani kumhifadhi mnyama huyu, ndani ya kitu kinachokaa kama gareji. Ilikuwa vyema kumwondoa katika hali hii,” akasema afisa wa wanyama.

Iliwabidi maafisa hao kumdunga dawa za kummaliza nguvu mnyama huyo ili wamwondoe kutoka eneo hilo.