Kimataifa

Aliyewaua Waislamu 6 msikitini kusamehewa baada ya miaka 40

February 11th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME raia wa Ufaransa na Canada ambaye aliwapiga wanaume sita wa Kiislamu risasi na kuwaua katika msikiti mnamo 2017 alihukumiwa kifungo cha miaka 40 gerezani.

Alexandre Bissonnette alifungwa Ijumaa na Jaji Francois Huot, watu wa familia na marafiki zake wakiachwa kwa vilio kortini.

Mwanamume huyo wa miaka 29 alikiri makosa hayo ya mauaji na majaribio sita ya mauaji mnamo Machi mwaka 2018.

Zaidi ya watu 50 walikuwa katika msikiti huo wakati alipofanya hivyo mnamo Januari 2017, alipoingia na kuanza kupiga marisasi walipokuwa katika maombi ya jioni.

“Naaibika kwa kile nilichofanya,” anaripotiwa kusema wakati huo, alipofikishwa kortini.

Alifungwa maisha, lakini akaambiwa anawezakujaribu bahati ya kuachiliwa kwa huruma ya Rais, japo baada ya kuozea gerezani miaka 40.

Alipokuwa akitoa uamuzi wake, Jaji huyo alisema kuwa siku hiyo ya mauaji milele “itasalia kuandikwa kwa damu katika historia ya Jiji hili, mkoa huu, nchi hii.”

Mshtakiwa alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu na alifahamika kwa kupinga vikundi vya kigaidi vikali hadi katika mitandao ya kijamii.

Upande wa mashtaka ulikuwa umependekeza kuwa afungwe maisha mara sita mfululizo, kumaanisha kuwa angepewa upenyu wa kutafuta kuachiliwa kwa huruma ya Rais baada ya miaka 150 jela.

Wakili wake naye alikuwa amehoji kuwa anafaa kuruhusiwa kuhurumiwa baada ya kukaa jela miaka 25, akisema kufungwa miaka 50 ama zaidi ungekuwa unyama na adhabu isiyo ya kawaida.

Aliua wanaume sita wa umri kati ya miaka 39 na 60, katika ibada iliyogeuka kuwa mauti na giza katika historia ya jiji hilo.