Kimataifa

Aliyewaua watu 12 kwa baa California apatikana amefariki

November 8th, 2018 2 min read

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

THOUSAND OAKS, Amerika

MWANAMUME mmoja ambaye alikuwa na bunduki aliwaua watu 12, akiwemo afisa wa polisi, alitekeleza shambulio la risasi katika baa moja ambako muziki huchezwa na iliyojaa wanafunzi wa vyuo katika jimbo la California, maafisa na mashahidi walisema Alhamisi.

Polisi walisema mshambuliaji huyo alipatikana amefariki ndani ya baa hiyo iliyoko viungani kwa jiji la Los Angeles. Hata hivyo, haikubainika iwapo aliuawa na maafisa hao wa usalama au alijipiga risasi.

Akiongea na wanahabari mapema Alhamisi, afisa mmoja wa polisi alisema takriban  watu 12 walijeruhiwa katika shambulio hilo. Alisema nia ya shambulio hilo wala asili ya mshambuliaji bado haijulikani.

Hicho ni kisa cha pili aina hiyo kutokea nchini Amerika kwa kipindi cha majuma mawili.

Mashahidi walisema walisema mshambuliaji huyo alikuwa amevalia koti jeusi. Kabla ya shambulio hilo mwanamume huyo alirusha gruneti la moshi ndani ya baa ya Borderline Bar and Grill, kabla ya kuanza kufyatua risasi humo mwendo wa saa tano na dakika 20 Jumatano usiku.

“Ni mandhari ya kuogofya. Kuna damu kila mahali,” Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Ventura Geoff Dean aliwaambia wanahabari.

“Hatuna habari kama kama kisa hiki kinaweza kuhusishwa na ugaidi au la. Kama mjuavyo, uchunguzi unaendelea na maelezo yatatolewa baada ya mshukiwa kutambuliwa na lengo lake kubainika,” akaongeza.

Dean alisema polisi aliyefariki na aliyetambuliwa kama Ron Helus, ambaye amehudumu katika jeshi hilo kw miaka 29, ndiye alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio.

“Tuliwapata watu 11 ambao walikuwa wameuawa,” akaeleza Dean akiongeza kuwa takwimu hiyo ilitolewa kabla ya kubainika kwa polisi huyo pia alikuwa ameuawa.

Hafla ya wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ilikuwa ikiendeshwa eneo la tukio liloko kitongoji cha Thausand Oaks. Mamia ya waru pia walihudhuria, akasema Kapteni Garo Kuredijian wa afisi ya Mkuu wa Usalama katika kaunti ya Ventura.

Matt Wennerstron, 20, mwanafunzi ambaye hupenda kuhudhuria hafla ya muziki katika baa hiyo alisea kuwa mshambuliaji huyo alifyatua risasi kwa kutumia bastola ambayo ilionekana kuwa na kati ya risasi 10 na 15.

Siku 10 zilizopita mwanamume mmoja mwenye bundukio aliwaua watu 11 ambao walikuwa wamehudhuria ibada katika kanisa moja eneo la Pittsburgh.

Shambulio hilo lilisemekana kuchochewa kisiasa kwa sababu mshukiwa Robert Bowers alisema alilenga kuwaua Wayahudi. Hii ni kwa mujibu wa kundi moja la kutetea masilahi ya Wayahudi ambalo limekuwa likipigwa na Rais Donald Trump.

Mwaka jana tamasha ya muziki kwa jina Route 91 jijini Las Vegas ilikuwa uwanja wa mashambulio mabaya ya halaiki katika historia ya Amerika. Mshambuliaji alifyatua risasi akiwa katika orofa ya 32 ya jengo la hoteli na Casino na kuwaua watu 58.