Habari Mseto

Aliyezaba polisi kofi atozwa faini Sh500,000 au jela miaka mitano

November 1st, 2019 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

MAHAKAMA ya Lamu imemtoza faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani mwanamume aliyepatikana na hatia ya kumzaba kofi afisa wa polisi na kisha kurarua sare yake wakati akijaribu kukwepa kukamatwa.

Kalume Ngumbao alitekeleza kosa hilo mjini Lamu mnamo Mei 1, 2019.

Maafisa watatu wa polisi walikuwa wametumwa kwenye makazi yake kumkamata kwa kufuata amri ya korti baada ya mshukiwa kutoroka na kujificha kwa miezi minane pindi alipopewa dhamana kuhusiana na kesi ya awali iliyokuwa ikimkabili.

Bango la kuelekeza wanaotaka kufika katika mahakama Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Mahakama ya Lamu iliafikia kutoa amri ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo baada ya kukosa kuhudhuria kikao chochote mahakamani katika kipindi chote cha miezi minane ambacho ni kinyume na matakwa ya dhamana yake aliyokuwa amepewa.

Mshukiwa alianza kuwatisha kwa maneno polisi na kisha kumwandama mmoja wao aliyemkamata na kuanza kumvurumishia makonde na kuchanachana sare yake.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba, amesema mshukiwa tayari alikuwa na historia chafu ya kufungwa miaka mitatu kwa makosa mawili ya awali ya kujipatia fedha takribani Sh300,000 kimagendo mnamo 2017.

“Umepatikana na hatia ya kudinda kukamatwa na maafisa watatu wa polisi waliokuwa wakitekeleza amri ya mahakama ya kukukamata. Pia umepatikana na hatia ya kumpiga kofi polisi na kurarua sare yake wakati ukijaribu kukataa kukamatwa. Mahakama imekutoza faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani. Una siku 14 za kukata rufaa,” akasema Bw Temba.