Michezo

Allan Wanga ateuliwa kocha kuiokoa Homeboyz

January 29th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa zamani wa Harambee Stars Allan Wanga ameteuliwa kama kocha mkuu wa Kakamega Homeboyz baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo raia wa Uganda Paul Nkata kufutwa kazi.

Mmiliki wa klabu hiyo Cleophas Shimanyula alitangaza kuteuliwa kwa Wanga kudhibiti chombo cha klabu hiyo ambacho kimekuwa kikisuasua msimu huu wa 2019/20.

“Ndiyo ni ukweli kwamba Allan Wanga ndiye kocha wetu mpya. Hata hivyo anachukua wadhifa huo kama kocha mshikilizi hadi tupate kocha mpya wa kupokezwa kandarasi ya kudumu. Paul Nkata hayuko nasi tena na tutawaelezea sababu za kutimuliwa kwake baadaye,”

“Bado tunalenga kuimarisha timu yetu na hata tunataka ifanye vizuri zaidi katika mechi za ligi kuu ya KPL,” akasema Nkata.

Kocha huyo ambaye mwanawe Nkata Juniour husakatia Bandari FC, alitimuliwa baada ya timu ya Kakamega Homeboyz kuagana sare tasa na Ulinzi Stars katika mechi ya ligi ya KPL Jumapili Januari 27 kwenye uga wa Bukhungu, kaunti ya Kakamega.

Kibarua cha kwanza kwa straika huyo wa zamani wa timu za AFC Leopards na Tusker FC ni mechi kali ya KPL dhidi ya Bandari Jumatano Januari 30 ugani Mbaraki mjini Mombasa.