Michezo

Allegri akataa ofa ya kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund

July 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Juventus, Massimiliano Allegri, amekataa ofa ya kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Allegri, 52, hajakuwa na klabu tangu alipoagana na Juventus mwishoni mwa msimu uliopita na nafasi yake kutwaliwa na aliyekuwa mkufunzi wa Chelsea, Maurizio Sarri.

Licha ya kuhusishwa na klabu nyingi katika kipindi hicho, Allegri alikataa ofa za kurejea uwanjani na kusisitiza kwamba muhimu zaidi kwake wakati huo ni kutulia na familia yake.

Ilikuwa hadi Julai 1, 2020, ambapo Allegri alifichua maazimio ya kurejea tena uwanjani, na ofa ya kwanza kumjia ikawa ile ya kudhibiti mikoba ya Dortmund ambao wameanika azma ya kuagana na mkufunzi Lucien Favre.

Hata hivyo, Allegri alitupilia mbali ofa hiyo na kusisitiza kwamba anapania zaidi kunoa kikosi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Katika mahojiano yake na La Gazetta dello Sport nchini Italia, Allegri alikiri kwamba kubwa zaidi katika mipango yake ni kutua uwanjani Old Trafford kuwatia makali vijana wa Manchester United.

Licha ya kuwaongoza Juventus kutia kapuni mataji matano ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika kipindi cha miaka mitano ya ukocha wake, Allegri alitimuliwa kwa kushindwa kuongoza miamba hao kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Chini ya ukufunzi wake, Juventus walizidiwa maarifa na Barcelona kwenye fainali ya UEFA mnamo 2015 kabla ya kuangushwa tena na Real Madrid mnamo 2017.

Hadi alipokabidhiwa mikoba ya Juventus, Allegri alikuwa pia amenoa vikosi vya AC Milan, Cagliari na Sassuolo.