Michezo

Allegri, Lampard, Vieira sasa pazuri kumrithi Sarri Chelsea

June 4th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Maurizio Sarri kwa sasa anajiandaa kubanduka kambini mwa Chelsea baada ya kuhudumu uwanjani Stamford Bridge kwa kipindi cha msimu mmoja pekee.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia, Sarri tayari amekubali kupokezwa mikoba ya Juventus ambao wamekuwa wakijivunia ukiritimba katika soka ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Atakuwa akilijaza pengo la mkufunzi Massimiliano Allegri ambaye alitemwa na Juventus mnamo Mei 2019 licha ya kuwaongoza waajiri wake hao kunyanyua ubingwa wa taji la Serie A kwa mwaka wa nane mfululizo.

Iwapo atavunja ndoa yake na Chelsea, basi miamba hao wa soka ya Uingereza waliotawazwa mabingwa wa Europa League msimu huu watakuwa na kibarua kigumu cha kujaza pengo la Sarri.

Ingawa hivyo, magazeti mengi nchini Uingereza yamefichua kwamba Allegri anaongoza orodha ya wakufunzi ambao Chelsea wanawamezea kwa sasa.

Kulingana na gazeti la The Sun, kocha huyo kwa sasa anajifunza Kiingereza na amekiri kwmaba ana msukumo wa kutia makali kikosi cha haiba kubwa katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Iwapo watashindwa kumshawishi Allegri kujiunga nao, Chelsea watapania kumwendea aliyewahi kuvalia jezi zao kati ya 2001 na 2014.

Frank Lampard. Picha/ Maktaba

Lampard kwa sasa anadhibiti mikoba ya kikosi cha Derby kinachoshiriki Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza.

Lampard amejivunia msimu maridhawa katika kampeni za Derby msimu huu na ilikuwa hadi siku ya mwisho wa msimu ambapo kikosi chake kilizamishwa na Aston Villa kwenye fainali ya mchujo wa kupanda ngazi kushiriki kivumbi cha EPL msimu ujao.

Veterani

Makocha wengine wanaohusishwa na mikoba ya Chelsea ni veterani wa zamani wa Arsenal Patrick Vieira, Diego Simeone wa Atletico Madrid na Nuno Espirito Santo aliyewatambisha Wolves vilivyo katika kampeni za EPL muhula huu.

Baada ya kuhusishwa kwa kipindi kirefu na Arsenal na Man-United hapo awali, huenda Simeone akahiari kutua kambini mwa Chelsea iwapo nyota Antoine Griezmann atashawishika kujiunga ama na Barcelona au Man-United wanaoyahemea maarifa yake.

Espirito mwenye umri wa miaka 45 anakamilisha orodha ya wakufunzi wanaoviziwa na Chelsea baada ya kuwaongoza Wolves kutinga nafasi ya saba kwenye jedwali la EPL mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Mbali na kuwaangusha miamba wengi katika soka ya EPL msimu huu, Espirito pia aliwaongoza vijana wake kutinga nusu-fainali ya Kombe la FA iliyowashuhudia wakizimwa na Watford.