Michezo

Amani, Beijing Raiders zakosa maarifa

March 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Amani Queens iliona giza iliporandwa bao 1-0 na Carolina for Kibera kwenye mchezo wa kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) uliyochezewa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Nayo Uweza Women FC kwa mara ya kwanza iliinyamazisha Beijing Raiders kwa mabao 2-1 baada ya Salome Mangera kucheka na nyavu mara mbili.

Carolina for Kibera ya kocha, Dennis Odhiambo ilishusha mchezo safi huku wachezaji wake wakionekana kujiaini wanaweza kulipua wapinzani wao.

Amani Queens ni kati ya vikosi vilivyotesa msimu uliyopita licha ya kuteleza dakika za mwisho na kulemewa kunasa tiketi ya kusonga mbele. Nahodha Sarah Sifuna wa Carolina for Kibera aliongoza wenzake na kutenda kweli kupitia bao lililofumwa na Cynthia Akinyi.

”Mechi hiyo ilishuhudia ushindani mkali mbele ya wapinzani wetu lakini Mungu ni mwema hatimaye tulifanikiwa kubeba alama tatu muhimu,” alisema nahodha huyo.

Naye bosi wa Amani Queens, Ben Ooko alisema ”Tulizabwa na washiriki wapya lakini wachezaji wangu waliwatoa kijacho chembamba.”

Kipute hicho pia kinajumuisha UoN Queens, Kibagare Girls, Achievers Ladies, Patriots Queens na City Queens kati ya zingine.