Amani: Museveni aombwa atumie busara Sudan Kusini

Amani: Museveni aombwa atumie busara Sudan Kusini

Na AFP

SHIRIKA la Maendeleo na Tawala za Kieneo (IGAD) limemwomba Rais wa Uganda Yoweri Museveni atumie hekima na uzoefu wake katika masuala ya uongozi ili kusaidia kutatua ukosefu wa usalama nchini Sudan Kusini.

Taifa hilo changa limekuwa likikabiliwa na utovu wa usalama huku makabila yakipigana na kuzozania rasilimali za kitaifa. Kando na hilo, Sudan Kusini imekuwa ikipitia misukosuko ya uongozi kati ya wanasiasa wakuu wa nchi hiyo.

Mjumbe wa IGAD wa Sudan Kusini Ismail Wais jana alimrai Rais Museveni ambaye ameongoza Uganda tangu 1986, aingilie kati na kuipa Sudan Kusini ushauri kuhusu mbinu za kupata amani.

“Hili eneo linakuhitaji mheshimiwa Rais. Kutokana na uzoefu wako na ushauri wako, Sudan Kusini itakuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mataifa mengine. Nchi yetu lazima iwe na mabadiliko na tunakuomba utusaidie kwa hili,’ akasema Wais jijini Kampala.

Mjumbe huyo alisema kuwa vita vya kikabila vimelemaza maendeleo nchini humo, huku pia akimtaka Rais Salva Kiir ashirikiane na viongozi wengine wa kimataifa kusaidia kujenga upya nchi hiyo na kuzima ghasia za kikabila kupitia mazungumzo.

Sudan Kusini ndiyo taifa changa zaidi Afrika baada ya kujitenga na Sudan na kuwa nchi huru mnamo 2011. Hata hivyo, kumekuwa na mzozo wa uongozi kati ya Rais Kiir na Naibu wake Riek Machar.

Uhasama wa kisiasa umeiponza nchi hiyo pakubwa huku Machar akiunda jeshi la upinzani maarufu kama SPLA-IOKwa upande wake, Rais Museveni alionekana kuridhia ombi hilo ila akasema suluhu ya kudumu ni kuandaliwa kwa uchaguzi wenye uwazi ambao hautaingiliwa na mrengo wowote wa kisiasa.

‘Kama kiongozi huwezi kushinda uchaguzi iwapo unaeneza chuki za kikabila kujitafutia umaarufu. Anayesaka uongozi lazima atakuwa kwenye muungano na viongozi wa maeneo mbalimbali. Atapataje kura miongoni mwa makabila ambako anahubiri chuki na kuyagonganisha?’ akauliza Museveni.

‘Sudan Kusini iandae uchaguzi huru inayofuata katiba na mshindi halali apatikane. Jeshi lisitumike kuwalazimisha raia wapige kura kwa mkondo fulani nakuvuruga kura. Hiyo ndiyo suluhu inayohitajika Sudan Kusini,’ akaongeza.

Aidha kiongozi huyo alishauri Sudan Kusini ianze kuwapa mazoezi ya kijeshi, wanajeshi wote kwa pamoja huku akisema hilo litasaidia kuzima mirengo inayochipuka ya maasi.

“Hapa hatukulipa jeshi kwa sababu hatukuwa na fedha zozote. Badala ya pesa, hakikisha wanajeshi wanatimiziwa masuala ya kimsingi kisha na pia kuraiwa wawe wazalendo,’ akasema Rais Museveni.

You can share this post!

Mjukuu wa Moi akubali watoto aliokana awali

Sheria njiani kupunguza walinzi wa DP hadi 30