Makala

MALEZI: Amani ya kesho inategemea malezi ya sasa kwa watoto

July 23rd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAHATMA Karamchad Gandhi, wakati akiwa hai aliwahi kusema kuwa ikiwa dunia ilikuwa na nia ya kupambana na ghasia za kila aina, haikuwa na budi kuwekeza rasilimali zake katika utunzaji na ulezi wa watoto.

“Watoto ndio kioo cha utiifu kwa amani. Hawana doa la ubaguzi; doa hilo huwekwa katika malezi. Watoto ni kioo cha mapenzi na amani na ikiwa tunaenzi dunia iliyo tulivu, tulee watoto wetu katika msingi wa usafi wao wa kiakili, basi tutakuwa tunatoka kutoka amani ya vizazi tukiingia kwa amani ya vizazi,” akasema Gandhi.

Gandhi ambaye alizaliwa Oktoba 2, 1869, na akaiaga dunia Januari 30, 1948, alikuwa mzawa wa taifa la India na ambaye aliongoza harakati za kushindia taifa hilo uhuru kutoka Uingereza.

Hali ya sasa ni tofauti kabisa ambapo wengi katika dunia wamekuwa wakilelewa katika mazingira ya ghasia, misukosuko ya kila aina na shaka za kesho kuhusu ujirani, hata watoto wamejipata wakiingizwa katika vita vya rasilimali na misimamo hasi ya kisiasa.

Kutoka kushoto: Marvin, Cliff na Rimmon katika picha hii waonekana wenye bashasha wakiwa Mjini Sabasaba, Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Wapo wachanganuzi ambao wanasema kuwa hali inaweza ikadhibitiwa na jamii ikajiweka katika mkondo wa kuwaondolea watoto kasumba za ghasia ili kunusuru kesho yao.

Aliyekuwa Kasisi Mkuu wa Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Nyeri, Peter Kairu anasema njia njema zaidi na ya uhakika ya kunusuru kesho yetu ni kupitia kuwapa watoto malezi bora.

Anasema kuwa hii sio ndoto bali ni wazo halali ambalo wanajamii hawajachelewa kuanza kulitekeleza.

“Angalia nyuso za watoto wanapoendelea na harakati zao za kimaisha. Waone jinsi huwa na hisia za upendo na kujituma kuwafaa watoto wenzao kwa hali na mali. Waone watoto hao wakicheza bila kuzingatia rangi ya ngozi zao, dini wala kabila. Hiyo ndiyo dunia ambayo tunaenzi kuipata na hatujachelewa,” anasema Kairu.

Anasema kuwa katika dunia ya sasa ambayo imejaa ukatili wa kila aina, watoto huwekwa kasumba katika bongo zao changa kuwa dunia ni hasi na haina nafasi ya amani.

“Ikiwa tungesusia hayo mabaya na tuzingatie kuwaweka watoto hawa imani kuwa jinsi wanavyosihi katika usafi wao wa kimawazo ndani ya uchanga wao ndivyo hali itaendelea kuwa hata wakikomaa, basi tutakuwa tumejinyakulia maana halisi ya amani,” anasema.

Anasema kuwa kuna ratiba ambayo inaweza ikakumbatiwa katika kuafikia dunia hii ya amani kupitia malezi bora.

“Kwanza tuwe tukiwahamasisha wote wanaojiingiza katika ndoa kuwa mapenzi kwa watoto watakaojaliwa na Maulana ndio kiingilio cha amani ya boma lao hata baada ya wao kuondoka katika uhai huu kwa kuwa mtoto atakalelelewa katika mazingara ya amani ataenzi amani na ataiendeleza kwa vizazi vyake,” anasema.

Anasema kuwa nao viongozi wa kidini wanafaa kuwa ngangari wakihubiri kuhusu imani kwa maisha hata wakati mambo yanaonekana wazi kwenda kombo.

Anasema kuwa kunafaa kuwe na msasa wa ni kina nani wanapewa wajibu wa kuwa wachungaji kwa kuwa kuna baadhi ambao ni wa kuitwa na Maulana, wengine wako katika riziki huku wengine wakiwa tu ni abiria katika safari ya kueneza injili ya maisha.

Ni wazo ambalo linakumbatiwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu nchini (Knut), Bw Wilson Sossion ambaye anasema udogoni, ni nadra kupata visa vya watoto kufanya maovu.

“Ni vigumu upate visa vya ghasia katika shule za chekechea na zile za msingi. Utovu huo wa nidhamu huanza kujipenyeza katika shule za sekondari, na taasisi za elimu ya juu,” anasema Sossion.

Anasema kuwa huo ni ushahidi kuwa malezi husambaratika jinsi miaka isongavyo katika uhai wa mtoto akilaumu jamii kwa kutozingatia malezi bora na kutoa mwongozo mwafaka wa kimaisha kwa watoto.

“Tumefeli kama ulimwengu katika malezi. Sisi wakubwa na wakongwe ndio kielelezo cha hawa watoto na yale ambayo unapata wakitekeleza, wameyasoma kutoka kwetu. Tubadili mienendo na tuwe tukijua watoto wanatuangalia wasome kutoka kwetu ndio tuzingatie tu yale ya kuwapa uthabiti wa mema maishani yao,” anasema.