Michezo

Ambaka atajwa kuwa 'mnyama akiwa na mpira' kwenye Vancouver Sevens

March 11th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA William Ambaka ni mmoja wa wachezaji saba mahiri sana na mwiba kwa wapinzani katika Raga za Dunia duru ya Vancouver nchini Canada za Machi 10-11, 2018.

Shirikisho la Raga duniani (World Rugby) limetia Mkenya huyu katika orodha hiyo likimtaja kuwa “mnyama akiwa na mpira na hatari kwa ngome yoyote”. “Kutokana na kasi yake na nguvu, mpinzani yeyote atajutia kumuachia nafasi ya kupenya.”

Ambaka amechezea Kenya mechi 27 msimu huu wa 2017-2018 akiifungia miguso 11 muhimu.

Wachezaji wengine ambao wametajwa na shirikisho hili kuwa hatari ni Jean Pascal Barraque (Ufaransa), Alasio Savita Naduva (Fiji), Folau Nuia (Marekani), Cecil Afrika (Afrika Kusini), Ben O’Donnell (Australia) na Danny Barrett (Marekani).

Kenya inafaa kuwa makini na orodha hii kwa sababu itakutana na Fiji na Ufaransa pamoja na Uhispania katika mechi za kundi C.

Katika jedwali la Raga za Dunia msimu 2017-2018, Fiji inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 79 nayo Kenya iko katika nafasi ya nane alama 34 nyuma. Ufaransa na Uhispania zinashikilia nafasi za 10 na 14 kwa alama 37 na 18, mtawalia. Kenya itafungua kampeni yake ya Vancouver Sevens dhidi ya Ufaransa hapo Jumamosi (9.14pm) na kulimana na Uhispania na Fiji usiku wa kuamkia Jumapili.