Kimataifa

Amekuwa jela miaka 28 baada ya mwanamke kuota kuwa alimbaka

June 20th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

DENVER, COLORADO, AMERIKA

MWANAMUME ambaye amekuwa jela kwa miaka 28 baada ya mwanamke kuota kuwa ndiye alikuwa amembaka anaweza kuachiliwa huru, baada ya mwanamume mwingine kukiri kuwa ndiye alifanya kosa hilo.

Clarence Moses-El alipatikana na hatia mnamo 1988 na akafungwa miaka 48 jela, kuwa alimbaka na kumchapa mwanamke alipofika nyumbani akitoka kulewa usiku.

Siku moja baada ya kudhulumiwa na wakati alikuwa hospitalini, mwanamke huyo alimtaja Moses-El kuwa ndiye alikuwa amemvamia, akisema sura yake ilimjia ndotoni.

Mfungwa huyo alikana kosa akisema hakufanya hivyo, lakini juhudi zake za kukata rufaa ya kosa hilo zikakosa kuzaa matunda, kwa kuwa polisi walitupilia ushahidi wa DNA uliohusishwa na tukio hilo.

Polisi waliteketeza mavazi ya mdhulumiwa na ushahidi mwingine licha ya Jaji kuamrisha kuwa uhifadhiwe kwa vipimo, ili kuonyesha ikiwa Moses-El alikuwa na makosa au la.

Lakini mnamo 2013, mwanamume mwingine kwa jina L.C Jackson alimwandikia mfungwa huyo barua akiwa jela, akisema hakuamini kuwa ndiye alimbaka mwanamke huyo, kwa kuwa alikuwa amefanya ngono naye wakati husika, usiku huo.

Barua hiyo ilisababisha kesi hiyo kusikizwa tena Julai, ambapo Jackson alitoa ushahidi kuwa alikasirika walipokuwa wakifanya ngono na mwanamke huyo na akamgonga usoni.

Mwanamke huyo alikuwa ameambia polisi kuwa alikuwa akilala wakati mwanamume alimwekelea mikono shingoni na akambaka.

Japo Jackson hajashtakiwa katika kesi hiyo, mnamo 1992 alifungwa kwa makosa ya kubaka mama na bintiye, wakati uchunguzi wa DNA ulionyesha kuwa aliwadhulumu hivyo. Kisa hicho kilitokea kama kilomita mbili kutoka nyumbani kwa mwanamke aliyesababisha Moses-El kufungwa.

Jaji aliyemfunga Moses-El ameamrisha Jackson apimwe na akipatikana na makosa, mfungwa Moses ataachiliwa huru. Ameamrisha kesi hiyo isikizwe tena.

Viongozi wa mashtaka wanapitia uamuzi wa korti uliotolewa wakati huo, wakilenga kukutana na mwanamke husika tena, kubaini ikiwa watafungua mashtaka mapya.