Shangazi Akujibu

Ameolewa na mwingine ilhali amekula pesa zangu nyingi

May 8th, 2024 1 min read

Vipi shangazi? Nimetumia pesa zangu nyingi kugharimia mahitaji ya mwanamke mpenzi wangu kwa sababu alikuwa ameniahidi atakuwa mke wangu. Sasa ameniacha akaolewa na mtu mwingine. Nifanyeje?

Hiyo ni hali ya mapenzi. Leo hapa, kesho kule. Ni haki ya mtu kubadili nia yake katika uhusiano wa kimapenzi na hata katika ndoa. Itabidi umsahau yeye na pesa ulizotumia kugharimia maisha yake.

Mpenzi aliyeahidi kunioa ni mkono birika mkubwa asiyekuwa na mfano

Hujambo shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitatu na ameahidi kunioa. Tatizo ni kuwa haonekani kujali kuhusu mahitaji yangu ya pesa. Ananipenda kweli?

Utakosea kushuku mapenzi ya mwenzako eti kwa sababu haonekani kujali mahitaji yako ya pesa. Labda hana uwezo. Na kama anao, huenda hajui mahitaji yako. Isitoshe, hiyo si lazima kwani ni mpenzi tu si mume wako.

Mchumba ameniacha baada ya kidudu mtu kunisingizia tabia mbaya

Kwako shangazi. Mpenzi wangu ameniacha baada ya mtu fulani kumwambia eti nina wanaume wengi katika mtaa ninaoishi. Mimi sina mwingine na hatua yake hiyo inaniumiza sana moyoni. Nishauri tafadhali.

Ni makosa makubwa kwa mpenzi wako kukuacha kwa kutegemea habari isiyo ushahidi. Kama kweli anakupenda angechukua muda kutafuta ukweli. Zungumza naye uone kama atabadili uamuzi wake. Akikataa achana naye, utapata mwingine.

Ni kama dada yangu ana nia ya kunipokonya mpenzi

Kwako shangazi. Ninashuku dada yangu anamnyemelea mpenzi wangu. Nilikagua simu yake nikagundua wamekuwa wakiwasiliana. Naogopa kumuuliza kwa sababu ni mkubwa wangu. Nishauri.

Una sababu ya kuwa na wasiwasi. Wawili hao hawana sababu nyingine ya kuwasiliana bila wewe kujua. Kama unaogopa kumuuliza dada yako, muulize mpenzi wako ujue kinachoendelea kati yao.