Kimataifa

Amerika inatuadhibu kwa kususia ushoga, Uganda yalia

June 4th, 2024 2 min read

KAMPALA, UGANDA

SERIKAI ya Uganda imepinga vikali vikwazo vipya ilivyowekewa na Amerika kwa ‘kisingizio’ cha kukithiri kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Ilisema Ijumaa vikwazo hivyo vinamlenga Spika wa Bunge, Anita Among na maafisa wengine waliounga mkono Sheria Inayoharamisha Ushoga 2023.

Alhamisi, Ubalozi wa Amerika ulitangaza vikwazo vya kusafiri na kifedha dhidi ya Among kwa sababu ya ufisadi unaohusu wadhifa wake wa uongozi.

Wengine waliowekewa vikwazo ni pamoja na mawaziri Amos Lugolobi, Agnes Nandutu na Mary Goretti Gitutu, kwa madai ya kutumia vibaya rasilimali za umma na kuelekeza kwingine bidhaa zinazonuiwa kufadhili jamii maskini zaidi nchini humo.

Waziri wa Masuala ya Kigeni nchini Uganda, Oryem Okello, alihoji kuwa mawaziri wote waliowekewa vikwazo kwa sasa wanakabiliwa na kesi kortini, ambazo bado hazitatoa uamuzi.

Vikwazo hivyo pia vinamlenga Luteni Jenerali Peter Elwelu kwa wajibu aliotekeleza katika vita baina ya vikosi vya usalama Uganda na kundi la wapiganaji nchini humo vilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya 100.

Hata hivyo, Okello alisema hatua ya serikali ya Amerika inamlenga hasa Among.

“Ninaamini hii ni kutukosea heshima na kudunisha idara yetu ya mahakama,” alisema Okello.

“Vikwazo hivyo si vya haki. Vinanuiwa kuadhibu,” alisema.

“Wanatukandamiza kwa sababu wanajua hatuwezi kufanya lolote kuhusu suala hilo. Na ni hatua ya kimaksudi kumwadhibu Spika kwa wajibu wake na uongozi katika kupiga vita LBGTQ na ushoga Uganda.”

Ubalozi wa Amerika umesema unasimama na raia wa Uganda kutetea kanuni za kidemokrasia, serikali inayohudumia wananchi wake wote na uwajibikaji kwa vitendo vilivyotekelezwa na wanaotumia vibaya nyadhifa zao kupitia ufisadi na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Mchanganuzi wa siasa Uganda, Mary Anne Nanfuka, alisema watu wanaolengwa na vikwazo hawafanyi kazi kivyao na kwamba vikwazo kamwe havifanikiwi kama vizingiti.

“Naona mataifa haya ya magharibi yanataka kuridhisha wapiga kura wao,” alisema Nanfuka.

“Wanajua vyema kuwa wanahitaji serikali ishirikiane nao katika sehemu fulani. Hivyo basi, mambo yatakapozidi unga, wataachana nayo. Naam, ni ishara, lakini la hasha, bado hatujaridhishwa,” alisema.

Mkuu wa Masuala ya Umma katika Bunge la Uganda, Chris Obore, alisema madai ya ufisadi ni ya kisiasa na ya kulipiza kisasi, la sivyo yangelenga baraza lote la mawaziri Uganda.

Ubalozi ulitaja msaada wa mabati yaliyodhamiriwa kusaidia jamii maskini ambao badala yake maafisa wakuu serikalini waligawana miongoni mwao.

“Ni ishara ya ghadhabu yao dhidi ya spika kwa kuongoza sheria ya kupiga ushoga,” alisema Obore.

“Ni wazi kuwa Uingereza, Amerika na Canada, zimekuwa zikishinikiza wakati sheria hiyo ilipokuwa ikijadiliwa. Kwa sababu haihusu mabati, Spika alinufaika vipi kibinafsi kutokana na mabati hayo wakati shule za umma zilizoezekwa ziko hapo?”