Kimataifa

Amerika kuchunguza mitandao ya kijamii ya wageni wote

June 2nd, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

RAIA kutoka mataifa ya nje watalazimika kutoa maelezo kuhusu akaunti zao za mitandao ya kijamii kabla ya kupokea Visa za kuwaruhusu kusafiri au kufanya kazi Marekani.

Idara ya uhamiaji nchini humo, jana lifichua kwamba wageni wanaotaka kuelekea Amerika watahitajika kuwasilisha majina wanayotumia kwenye mitandao ya kijamii, barua pepe pamoja na nambari za simu ambazo wamekuwa wakitumia kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, baadhi ya mabalozi na watu maarufu hawatalazishwa kupitia masharti hayo ambayo yataathiri karibu watu 14.7 milioni kila mwaka.

Watu wanaosafiri hadi Marekani kusoma au kufanya kazi hata hivyo ni lazima wazingatie agizo hilo jipya.

“Tunaendelea kufanya bidii kuhakikisha tunaimarisha mtindo wetu wa ukaguzi wa raia wanaotoka nje ili kuwalinda Wamarekani. Hata hivyo hatuwakandamizi watu wanaokuja Marekani kwa nia nzuri,” ikasema taarifa kutoka Idara hiyo.

Zamani watu waliohitajika kupitia ukaguzi huo mkali ni wale waliokuwa wakitoka mataifa yanayodhibitiwa na makundi ya kigaidi.

Hata hivyo, watu sasa watahitajika kuwasilisha majina ya akaunti zao kwenye mitandao ya kijamii na pia kutoa maelezo mengine kuwahusu kwa hiari.

Masharti haya mapya yalipendekezwa na serikali ya Rais Donald Trump mwezi Machi mwaka wa 2018.

Hata hivyo sheria hiyo imepingwa na kundi la wanaharakati kwa jina American Civil Liberties Union ambalo lilisema haitasaidia kuhakikishia Marekani usalama bali itasababisha wengi kudhibiti jinsi wanavyotumia mitandao yao.

Akifanya kampeni ya Urais mwaka wa 2016, Rais Donald Trump aliahidi kupambana na wahamiaji haramu wanaoingia nchini Marekani na akisema wageni watapitia ukaguzi wa kina kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Mnamo Ijumaa Rais Trump aliahidi kuwekea Mexico vikwazo iwapo haitadhibiti idadi ya wahamiaji wake wanaoingia Marekani kupitia mipaka ya mataifa hayo mawili.

Kwingineko, Trump anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu nchini Uingereza leo huku akiirai nchi hiyo kuharakisha kujiondoa kwenye Muungano wa Bara Ulaya (EU).

Kiongozi huyo ameieleza Uingereza isilipe Sh4 trilioni zinazohitajika kabla ya kugura EU kisha kumpendekeza aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni Boris Johnson ateuliwe Waziri Mkuu wakati Theresa May atakapojiuzulu Juni 7 baada ya bunge kukataa kuidhinisha mswada wa kuondoa Uingereza kwenye EU kutokana na utata kuhusu masuala kadhaa ya kiuchumi.