Amerika kupeleka tena wanajeshi wake Somalia

Amerika kupeleka tena wanajeshi wake Somalia

NA AFP

WASHINGTON, Amerika

RAIS wa Amerika Joe Biden ameamuru kupelekwa kwa wanajeshi wa nchi hiyo nchini Somalia kusaidia katika vita dhidi ya kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab, afisa mkuu wa Amerika amesema.

Hatua hiyo inakwenda kinyume na amri ya mtangulizi wake, Donald Trump, ambaye mnamo 2020 aliwaondoa wanajeshi wote wa Amerika kutoka Somalia.

Alifanya hivyo kama sehemu ya mpango wake wa kusitisha shughuli za wanajeshi wa Amerika katika mataifa ya kigeni wiki chache kabla ya kuondoka afisini.

“Rais Biden ameidhinisha ombi kutoka kwa Idara ya Jeshi kwamba wanajeshi wachache watumwe Somalia ili kusaidia katika vita dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab. Wapiganaji hao wamekuwa tisho la usalama katika taifa hilo la Mashariki mwa Afrika,” afisa huyo akasema Jumatatu.

Wanajeshi 500 ndio watatumwa nchini Somalia ambao pia watatoa mafunzo, na misaada mbalimbali, kwa wanajeshi wa Somalia.

Hii ni idadi ndogo ya wanajeshi ikilinganishwa na jumla ya wanajeshi 750 wa Amerika waliokita kambi nchini Somalia kwa miaka saba wakiendesha operesheni dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab.

Lakini waliondolewa na utawala wa Trump na baadhi yao wakatumwa katika mataifa jirani ya Kenya na Djibouti.

“Mnamo Desemba 2020, muda mfupi kabla ya kuondoka afisini, Trump aliamuru kuondolewa kwa wanajeshi wa Amerika kutoka Somalia kinyume na ushauri wa maafisa wakuu wa kijeshi,” afisa huyo akasema.

“Tangu wakati huo wanamgambo wa Al-Shabaab wameendeleza mashambulio yao,” afisa huyo akaongeza.

Afisa huyo alifafanua kuwa uamuzi huo wa Rais Biden hauna uhusiano wowote na uchaguzi wa Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, mnamo Jumapili.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya nchini hiyo kukumbwa na misukosuko ya kisiasa na janga la ukame. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Somalia wamekuwa wakiunga mkono ushirikiano kati ya wanajeshi wa Amerika na wale wa Somalia katika vita dhidi ya Al-Shabaab.

Afisa huyo alisema Amerika ina matumaini kuwa utawala mpya wa Rais Mohamud utaendeleza ushirikiano huo.

Huku akimpongeza rais huyo mteule, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken, alimtaka kujenga kikosi cha wanajeshi kitakachopambana vikali na wanamgambo wa AlShabaab.

“Aidha, Rais mpya wa Somalia anafaa kutwaa majukumu ya usalama ambayo sasa yanaendeshwa na Kikosi cha Usalama cha Umoja wa Afrika.

KUPUNGUZA HATARI

Kwa kurejesha wanajeshi wake nchini Somalia, Amerika itapunguza hatari iliyoko katika mtindo wa kuendesha operesheni za muda dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab nchini Somalia.

Hatua hiyo itaimarisha utendakazi wa vikosi maalum na kutoa nafasi kwa muda mrefu wa utoaji wa mafunzo kwa wanajeshi wa Somalia.

Mnamo Jumatatu msemaji wa makao makuu ya jeshi la Amerika, Pentagon, John Kirby alisema Waziri wa Ulinzi Lyloyd Austin hakuridhishwa na mfumo wa sasa unaotumiwa na wanajeshi wa Amerika nchini Somalia.

“Hii ndio maana Pentagon iliomba Rais Biden aamuru kurejeshwa kwa kikosi kamili cha wanajeshi kukita kambi nchini Somalia,” Kirby akasema.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal yapoteza tumaini

Karua alazimisha Ruto kufanya hesabu upya

T L