Amerika kushirikiana na utawala mpya 2022

Amerika kushirikiana na utawala mpya 2022

Na RUSHDIE OUDIA

AMERIKA imesema itaisaidia Kenya kuandaa uchaguzi huru na wenye haki mwaka 2022.

Hilo pia litaisaidia Kenya kuepuka uwezekano wa ghasia kuzuka baada ya uchaguzi huo.

Kupitia Kaimu Balozi wa Amerika nchini, Bw Eric Kneedler, taifa hilo lilisema limejitolea kushirikiana na utawala utakaobuni serikali baada ya uchaguzi huo, bila kujali yule atachaguliwa kama rais.

Balozi huyo alisema wananchi ndio wenye uwezo kufanya maamuzi kuhusu utawala wa nchi, hivyo lazima viongozi waheshimu maamuzi yao na yale ya mahakama.

“Lazima wananchi waanze kuwashinikiza viongozi kuwajibika kwani wana nguvu kufanya mabadiliko kupitia upigaji kura. Wapigakura wanafaa kutowachagua viongozi ambao wanahisi hawatekelezi majukumu wanayofaa. Badala yake, wanafaa kuwachagua viongozi wenye maadili,” akasema balozi huyo.

Bw Kneedler, ambaye alikuwa akihutubu jijini Kisumu kwenye kikao na wanahabari, alisisitiza kuhusu haja ya wadau wote kushirikiana kuhakikisha ghasia hazitatokea nchini kutokana na uchaguzi.

Akionekana kukwepa kuzungumzia sera ambazo wawaniaji mbalimbali wa urais wamekuwa wakiahidi kuzitumia kukuza uchumi, Bw Kneedler alisema ni jukumu la Wakenya kufanya maamuzi yatakayowafaa.

“Huu ni uchaguzi unaowahusu Wakenya na mustakabali wao. Lazima watathmini kwa kina ahadi wanazopewa kabla ya kuwachagua viongozi waliojitokeza,” akasema.

Alisema hilo litafikiwa ikiwa watu wengi zaidi watajitokeza kama wapigakura.

Jumla ya Wakenya 1.5 milioni walijisajilisha kama wapigakura kwenye zoezi lililoendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kati ya Oktoba na Novemba.

Aliwaomba vijana na watu wengine ambao bado hawajasajiliwa kujisajilisha, kwani hiyo ni haki yao kidemokrasia.

“Ninawaomba kujitokeza kusajiliwa kwa sababu ni kupitia hilo ambapo mtapata nafasi ya kuwashinikiza viongozi kuwajibika,” akasema.

Alisema kuwa kupitia mashirika mbalimbali, serikali ya Amerika itaunga mkono juhudi zote zinazolenga kuboresha mikakati ya matayarisho kuhusu uchaguzi huo. Juhudi hizo ni kama uzuiaji wa ghasia na kuwapa mafunzo wapigakura.

“Kenya na Amerika ni marafiki wa muda mrefu. Ushirikiano huo utaendelea kuwepo licha ya matokeo ya uchaguzi huo,” akasema.

Amerika pia ilisema iko tayari kuisaidia Kenya kukabiliana na athari zozote zinazohusiana na vita vinavyoendelea katika eneo la Tigray (Ethiopia) na Sudan Kusini.

Balozi huyo pia aliwarai Wakenya kujitokeza kupewa chanjo, akisisitiza kuwa taifa hilo litaendelea kuisaidia Kenya kupata chanjo zaidi dhidi ya virusi vya corona.

Alisema kuwa kufikia sasa, Amerika imetoa dozi 4 milioni za chanjo hizo kwa Kenya na mashine 200 za kuwasaidia waathiriwa wa virusi hivyo kupumua.

“Tunaelewa kuna habari nyingi za kupotosha ambazo zinaenezwa kuhusu chanjo hizo. Hata hivyo, tunawahakikishia wananchi kuzipuuza,” akasema. 

You can share this post!

Uhuru apigia debe Raila kumrithi 2022

Jinsi ya kutunza vidole na kucha

T L