Amerika mbioni kumtimua Trump

Amerika mbioni kumtimua Trump

Na MASHIRIKA

WABUNGE wanatarajiwa kupiga kura leo usiku kupitisha hoja ya kuidhinisha Makamu wa Rais Mike Pence kumtimua Rais Donald Trump kwa kuchochea vurugu wiki iliyopita. Hii ni hatua ya kumzima Trump kuwania urais tena hapo 2024.

Spika wa Bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi jana alishikilia kuwa ni sharti Trump atimuliwe kwa kuchochea wafuasi wake kuvamia Jengo la Bunge la Capitol Hill.

Wabunge wanataka Pence atumie Kifungu cha 25 cha Katiba kinachomruhusu kutangaza Trump kama mtu asiyefaa kushikilia afisi ya umma. Lakini ripoti zinaonyesha kuwa Pence hakubaliani na pendekezo hilo la kumtaka kutimua Trump.

Watu watano, akiwemo afisa wa polisi aliyekuwa akilinda jingo la bunge, waliuawa wakati wa vurugu hizo. Trump wa chama cha Republican, hajatoa tamko lolote kuhusu wito wa Pelosi kutaka atimuliwe.Trump amesalia mpweke tangu Ijumaa alipopigwa marufuku kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii, ikiwemo Twitter na Facebook.

Trump anatarajiwa kuondoka afisini Januari 20 – siku ambayo Joe Biden ataapishwa kuongoza Amerika kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Trump tayari amesema kuwa hatahudhuria sherehe ya kumwapisha Trump.

Meya wa jiji la Washington, Muriel Bowser ameitaka wizara ya Usalama kuimarisha ulinzi katika eneo ambapo hafla ya kumwapisha Biden itaandaliwa kutokana na hofu kuwa huenda wafuasi wa Trump wakazua fujo katika ukumbi huo.

Bi Pelosi alisema kuwa aliwaandikia barua wabunge akisema kuwa, bunge litamkabidhi Pence hoja ya kumuidhinisha kutimua Trump leo.Baada ya kukabidhiwa uamuzi wa Bunge, Pence pamoja na baraza la waziri watapewa muda wa saa 24 kumchukulia hatua Trump.

Iwapo watakosa kumuondoa, wabunge watapiga kura kwa mara nyingine na kumtimua. Uamuzi wa wabunge baadaye utapelekwa katika Seneti ambapo atachunguzwa na kisha kupiga kura.

Maseneta wengi wakiunga mkono hoja ya kumtimua, Trump hataruhusiwa kuwania tena katika siku za usoni. “Inafaa tuchukue hatua za haraka kwa sababu Trump ni tishio kwetu na demokrasia ya Amerika,” akaandika Pelosi.

Japo Pence ametangaza kuwa atahudhuria hafla ya kumwapisha Biden pamoja na makamu wa rais Kamala Harris, hajaonyesha nia ya kuitikia wito wa kumtaka kutimua Trump.Baadhi ya maseneta wa chama cha Republican, akiwemo Seneta wa Pennsylvania, Pat Toomey, wamemtaka Trump kujiuzulu ili kujiondolea aibu ya kutimuliwa.

Mkewe Rais Melania Trump jana alishutumu vurugu zilizotokea wiki iliyopita huku akisema kuwa demokrasia ya nchi hiyo inafaa kudumishwa.

‘Ninawasihi mjitenge na vurugu. Msiumizane kwa sababu ya siasa au misingi ya rangi,” akasema Melania Trump.Pelosi alisema kura ya kumtimua Trump itafanyika katikati mwa wiki hii endapo Pence atashindwa kuchukua hatua.

You can share this post!

Maraga asifiwa kwa kuongeza idadi ya korti nchini

Jeshi lamwagwa miji mikuu uchaguzi mkuu ukinukia