Habari

Amerika yaamua

November 3rd, 2020 3 min read

Na DOUGLAS MUTUA akiwa Washington DC, AMERIKA

RAIA wa Amerika wamepanga foleni ndefu leo Jumanne kuchagua ni nani atakayekuwa Rais wao kwa miaka minne ijayo kati ya Rais Donald Trump wa chama cha Republican na mwaniaji wa chama cha Democrat Joe Biden.

Hadi kufikia Jumatatu, karibu kura milioni 100 zilikuwa zimepigwa mapema ama kwa njia ya mtu binafsi au kupitia njia ya posta.

Kikawaida, Waamerika walio nje ya nchi au wasioweza kufika vituoni kupiga kura huruhusiwa kuzituma kwa posta.

Hata hivyo, baadhi ya majimbo huruhusu watu kupiga kura mapema, yapata miezi miwili hivi kabla ya siku ya uchaguzi, kama njia moja ya kuhakikisha wasiopata nafasi siku ya uchaguzi hawakosi kushiriki shughuli hiyo.

Mwaka huu watu wengi zaidi wamepiga kura mapema kwa sababu tatu: hofu ya ugonjwa wa korona, msisimko wa kampeni na kulegezwa kwa sheria na kanuni kali kwenye majimbo mengi ambayo awali yaliyowazuia wengi.

Kutokana na kuzuka kwa janga la Covid-19 sheria hizo zimelegezwa ili watu wapige kura mapema badala ya kusongamana vituoni na kuhatarishiana afya siku ya leo.

Ushindi wa Trump utakuwa na maana kwamba ataendelea na sera zake za kuikweza Amerika juu ya mataifa yote duniani akitumia kauli-mbiu ya ‘Amerika Kwanza!’

Kwa mfano, anatatajiwa kuendeleza vita vya kiuchumi dhidi ya Uchina, ambavyo tayari vinawaathiri vibaya wakulima wa Marekani ambao huuza mazao yao Beijing.

Tayari bei za baadhi ya bidhaa zimepanda nchini Amerika kwa sababu Uchina nayo imeacha kuiuzia vitu kama vyakula na vifaa vya teknolojia.

Ikiwa Bw Biden atashinda, Amerika itaanza safari ndefu ya kukarabati uhusiano wake na jamii ya kimataifa ambao umeharibiwa vibaya tu na maamuzi ya Trump.

Biden akishinda, mahusiano ya kidiplomasia kati ya Amerika na mataifa mengine yatarejea.

Biden ameahidi: “Nitarejesha kuaminika kwa Amerika na washirika wetu wa Uropa na wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO.”

Kwa jumla, ushindi wa Biden utarejesha ustaarabu na hadhi kuanzia Ikulu ya White House hadi ngazi ya kimataifa.

Aibu ndogondogo kama kisa ambapo Trump alinukuliwa akiyaita mataifa ya Afrika ‘mashimo ya choo’ hazitarajiwi kutoka kwenye kinywa cha Biden kwa sababu anaheshimu watu wote.

Hakika, Waafrika wengi waliohamia Amerika wanamuunga mkono Biden kwa sababu walichukizwa sana na matusi ya Trump pamoja na vitisho vyake kwamba atawapokonya uraia.

Misaada ya kimataifa ambayo Marekani huyapa mataifa yanayoendelea ili kukabiliana na changamoto za afya itarejelewa. Mathalan, mfuko wa Wakfu wa Rais wa kikabiliana na Ukimwi (PEPFAR) ambao uliyafaa zaidi mataifa ya Afrika kabla ya Trump kuingia mamlakani unatarajiwa kuzinduliwa upya.

Kwa Wamarekani, ushindi wa Trump utakuwa na maana kwamba uchumi wa nchi utapewa kipaumbele badala ya afya.

Hizo ni habari mbaya kwa raia wa nchi hii ambayo ina idadi kubwa zaidi duniani ya vifo na wagonjwa wa Corona.

Rais Trump amekuwa akisisitiza kwamba karantini au udhibiti wowote ule kwa ajili ya ugonjwa wa Corona unahujumu uchumi wa nchi kwa sababu biashara nyingi zimefungwa na nyingine zikafilisika.

Amenukuliwa akisema si hoja kwamba watu wamefatiki kwa wingi kutokana na Corona, eti Wamarekani wanapaswa kuzoea kuishi na ugonjwa huo kabla ya tiba au chanjo kupatikana.

Biden, ambaye anasifika kwa kulia na wanaoomboleza, anatarajiwa kuwaliwaza waathiriwa wa korona na kuwapa matumaini kwamba afya siku za baadaye zitakuwa bora.

Trump amekuwa maarufu miongoni mwa wafuasi wake kwa kuwapuuzilia mbali wanasayansi na wataalamu wa afya kwa jumla akisema wanayafanya maisha ya watu kuwa magumu mno.

Kwenye ngazi ya kimataifa, Trump alikwisha ondoa mchango wa Marekani kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) hatua ambayo ilishangiliwa na wafuasi wake na kulaaniwa na upande wa Bw Biden.

Mshindi wa uchaguzi huu atategemea zaidi kura za majimbo machache ambayo hufuata upepo wakati wa uchaguzi badala ya kuunga mkono chama kimoja daima.

Majimbo hayo ni Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Ohio, Virginia na kadhalika. Wajumbe kutoka majimbo haya machache ndio watakaomwezesha mmoja wa wawaniaji hao kutua Ikulu.

Kwa mujibu wa kura za maoni, karibu yote haya yanamuunga mkono Biden.

Yapo ambayo huitwa ‘majimbo ya bluu’ (rangi ya chama cha Democrat) ambayo daima ni ya chama cha Democrat. Makuu kati ya hayo ni pamoja na California, Connecticut, Delaware, Hawaii, Illinois, Maryland, Massachusetts, Minnesota, New Jersey, New Mexico, New York, Oregon, Rhode Island na Vermont na Washington.

Vile vile kuna ‘majimbo mekundu’ (rangi ya chama cha Republican) ambayo kikawaida ni ya chama cha Republican, nayo ni Texas, Missouri, Arizona, Alabama, Alaska, Idaho, Kansas, Montana, Nebraska, North Dakota, Oklahoma na kadhalika.