Habari

Amerika yaanza mchakato rasmi kujiondoa katika makubaliano ya mazingira ya Paris

November 5th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

Na WASHINGTON D.C., AMERIKA

AMERIKA imetaarifu Umoja wa Mataifa (UN) kwamba inataka kujiondoa rasmi katika Mkataba wa Makubaliano ya Uhifadi Mazingira ya Paris, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Kigeni Mike Pompeo aliyeandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter mnamo Jumatatu.

Ikifaulu itakuwa ni nchi ya kwanza kujiondoa kwa makubaliano hayo yaliyofikiwa mwaka 2015 na yanayolenga kudhibiti kiwango cha gesi chafu inayotolewa.

Hili litakuwa ni pigo kwa wanachama wengine wanaohisi kwamba Amerika chini ya utawala wa Rais Donald Trump inakuwa yenye kupinga makubaliano hayo, ikiwa tofauti kabisa na enzi ya utawala wa Barack Obama aliyetangaza kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa hadi ya asilimia 26 na 28.

Uamuzi huu wa Amerika ni hatua ya mwanzo ya mchakato wa mwaka mzima utakaokamilika Novemba 4, 2020.

Wanamazingira wanaonya kwamba hatua ya Amerika kujiondoa huenda ikawa na athari hasi duniani.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uchanya wa Viumbe – Center for Biological Diversity – Jean Su amesikitikia hatua ya utawala wa Trump.

“Trump anaweza kujiondoa katika mkataba wa Paris, lakini hawezi kujiepusha wala kukwepa athari za uchafuzi wa mazingira,” amesema Su.

 

Tineja wa Sweden Greta Thunberg amekuwa mstari wa mbele kuongoza vijana kuandamana kupinga uchafuzi wa mazingira.