Habari Mseto

Amerika yalalama madaktari wa Cuba wanateswa

October 1st, 2019 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

AMERIKA imeweka vikwazo vya usafiri dhidi ya maafisa wa Cuba inaodai kuwa, wanatumiwa na serikali kunyanyasa madaktari wake wanaohudumu ng’ambo.

Maafisa hao, inasemekana, hufuata maagizo ya serikali ya Rais Raul Castro kutumia kanuni za kiutumwa za leba dhidi ya madaktari hao, na mwishowe kutia mifukoni hela karibu Sh700 bilioni kila mwaka.

Kanuni hizo ni pamoja na kufanya kazi kwa saa nyingi kupita kiasi bila mapumziko, mshahara finyu, makazi yasiyo salama, na kuzuiwa kutembeatembea.

Serikali pia imetwaa pasipoti za madaktari hao. Vile vile, hupeleleza wanachokifanya siku za mapumziko.

“Kujinufaisha na jasho la madaktari wa Cuba imekuwa desturi ya miongo mingi ya uongozi wa akina Castro, na inaendelea hadi leo. Tunaweka vikwazo dhidi ya viza za maafisa husika wa Cuba kuambatana na Sheria ya Uhamiaji na Urais Ibara 212(a)(3)(C),” ilisema Idara ya Serikali ya Amerika katika taarifa Jumatatu.

Takriban madaktari 50,000 wa Cuba wanafanya kazi katika mataifa ya nje zaidi ya 60.

Kikosi hicho kinaenziwa kama bora zaidi cha madaktari kinachotumwa na serikali hiyo ya kikomunisti, kwa lengo la kuimarisha matibabu na afya katika mataifa yanayoendelea.

Kenya ni moja ya mataifa yanayonufaika na mpango huo baada ya kupokea madaktari 100 wa Cuba mwaka jana, licha ya pingamizi kutoka kwa Muungano wa Madaktari na Madaktari wa Meno (KMPDU).

Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Ouma Oluga alisema kuwa, kuwaleta madaktari hao nchini ni mzigo usiohitajika ambao utagharimu taifa zaidi ya Sh2 bilioni, pasipo kujumuisha gharama za usalama, usafiri, makazi na chakula kwa serikali za kaunti.

Amerika ilisema kuwa imepokea masimulizi ya moja kwa moja kutoka kwa madaktari waathiriwa, huku taarifa za baadhi yao zikiashiria kwamba walilazimishwa ili kwenda kuhudumu katika mataifa ya kigeni.

“Idara ya Serikali ya Amerika imenakili visa vya ulanguzi wa binadamu katika mpango wa Cuba wa kutuma madaktari katika mataifa ya kigeni, kila mwaka tangu Ripoti ya Ulanguzi wa Binadamu (TIP) ya 2010 na pia ripoti ya TIP 2019. Visa hivi vinazidi kutia wasiwasi,” ilisema idara hiyo.

Dkt Tatiana Carballo, ambaye alihudumu katika mpango huo nchini Venezuela kwa miaka saba na pia nchini Brazil, alisema kuwa walipokea tu asilimia 10-15 ya mshahara ambao mataifa hayo ya kigeni yaliwalipa.

Baadaye alijiondoa kutoka kwa mpango huo, hatua iliyomtia yeye na familia yake hatarini.

Pamoja na kufanya kazi kwa saa nyingi bila marupurupu ya ziada, serikali ya Cuba huwalazimu madaktari hao kutumia huduma zao kama kifaa cha kisiasa.

Amerika ilishutumu vikali jambo hilo ikisema kuwa mpango wowote wa afya unaoshurutisha, kuhatarisha, na kunyanyasa wajumbe wake uko na kasoro.

“Tunahimiza serikali zinazoshiriki katika mpango huo wa Cuba wa kutuma madaktari wake ng’ambo, kuhakikisha kuwa wanawalinda dhidi ya unyanyasaji wa kikazi,” taarifa ilisema.