Makala

Amerika yamkalia ngumu Ruto, yamtaka azime ufisadi wa wazi serikalini


BAADA ya kumkumbatia Rais William Ruto, Amerika sasa inamsukuma vikali ikitaka aonyeshe kwa vitendo kwamba serikali yake inakabiliana na ufisadi na kuheshimu haki za binadamu.

Amerika iliwasilisha ujumbe mkali kwa Rais Ruto kupitia waziri msaidizi wa Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu, Bi Uzra Zeya aliyezuru Kenya Jumanne na Jumatano wiki hii, siku moja kabla ya mawaziri wapya kuapishwa.

Haya yalijiri huku raia wakiandamana kushinikiza utawala bora na kuangamizwa kwa ufisadi serikalini.

Bi Zeya, alikutana na maafisa kadhaa wa serikali ya Kenya akiwemo Rais Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome.

Taifa Leo imebaini kuwa Amerika ilionya Kenya kuhusu viwango vya juu vya ufisadi wa wazi na unaoendelezwa wazi na maafisa wa umma ikiwemo kuuanika kupitia mitandao ya kijamii bila kuchukuliwa hatua.

Katika mkutano na Rais Ruto Jumanne, afisa huyo wa Amerika aliitaka Kenya kuchukua hatua dhidi ya maafisa wa serikali wanaopata utajiri wa haraka, na kukabiliana na ukatili wa polisi, duru ndani ya serikali zilithibitisha.

Bi Zeya mwenyewe alithibitisha kuwa aliitaka serikali ya Kenya kukomesha ukatili wa polisi na kuondoa maafisa wa serikali wanaohusika na ufisadi ambao wamepata utajiri wa haraka na kuutwaa urejeshewe umma.

“Tumeeleza kwa nguvu sana msimamo wetu kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Serikali ya Biden, kuanzia mwanzo ilizidisha vita dhidi ya ufisadi ulimwenguni na kuutaja kama tishio kwa usalama,” Bi Zeya alisema alipokamilisha ziara ya siku mbili nchini Kenya mnamo Jumatano.

“Kwetu, kipaumbele ni kutia nguvu taasisi zinazohusika na vita dhidi ya ufisadi na kuhakikisha wale wanaoshiriki uovu huo wanashtakiwa na utajiri wanaopora unarudishiwa watu wa Kenya.”

Vita dhidi ya ufisadi na mageuzi ya polisi zilisisitizwa katika mazungumzo kuhusu utawala na haki za binadamu wakati wa ziara ya Rais Ruto nchini Amerika mwezi Mei mwaka huu.

“Ninatazamia tutashirikiana kutekeleza hili na kuanza mageuzi ya vita dhidi ya ufisadi ili kuinua maadili ya demokrasia ambayo yanaunganisha nchi zetu pamoja,” Rais Biden alimweleza Rais Ruto walipokutana katika Ikulu ya White House mnamo Mei.

Nchi zote mbili zilitia saini makubaliano ya kuimarisha utawala na haki za binadamu huku Amerika ikiahidi kupatia Kenya Sh 65 milioni katika mpango wa “kuhakikisha michakato ya bajeti ya serikali za kaunti inakuwa yenye uwazi zaidi na shirikishi na kuongeza ushirikishaji wa umma.”

Amerika pia ilitangaza msaada mwingine wa Sh65 milioni “ kupanua na kuongeza ufanisi katika vita dhidi ya ufisadi kwa kuwezesha mashirika ya kijamii kuunda na kusambaza maudhui ya kushirikisha raia ili hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wafisadi.”

Amerika kwa kulenga kulinda wanaofichua ufisadi ilisema itatoa Sh33 milioni kupitia mpango wa Uwajibikaji Ulimwenguni na Sh40 milioni kusaidia sheria iliyopendekezwa ya kulinda wanaofichua ufisadi Kenya.

Hata hivyo, pesa hizi zingetolewa serikali ya Rais William Ruto ikionyesha kwa vitendo. Mnamo Ijumaa, Rais Ruto alisisitiza kuwa ufichuzi wa ufisadi ni muhimu kwa vita dhidi ya uovu huo.

“Tunaamini kwamba vita vyetu dhidi ya ufisadi vitapigwa jeki na hatua za kuzifanya kuwa rahisi na salama kwa raia na wafichuzi kujitokeza na kuripoti ufisadi na uhalifu wa kiuchumi. Kwa hili, baraza mpya la mawaziri litaandaa mageuzi ya sheria ya kulinda mashahidi ili kuiimarisha,” Rais Ruto alisema alipoongoza hafla ya kuapisha mawaziri 19.